.

Chanzo cha picha, Reuters

Iliyochapishwa

Muda wa kusoma: Dakika 5

Teknolojia ya Video Assistant Referee (VAR) tayari ilikuwa mada kubwa ya mjadala katika Kombe la Dunia la Wanaume la FIFA 2026, lakini mjadala huo ulizidi kuwa mkali baada ya ushindi wa kushangaza wa Argentina dhidi ya Misri katika hatua ya 16 bora tarehe 7 Julai.

Timu ya Misri, iliyokuwa inaongoza kwa mabao 2-0 huku zikiwa zimesalia dakika 11 kabla ya mwisho wa mchezo, ilishuhudia Lionel Messi akiiongoza Argentina kufunga mabao matatu ya haraka na kuibuka na ushindi. Baada ya mechi hiyo, Wamisri walionyesha hasira kubwa kufuatia bao lao moja kufutwa na madai yao ya penalti ya dakika za mwisho kupuuzwa, huku VAR ikiwa haikuingilia kati.

“Huenda walitaka mabingwa watetezi waendelee kwenye mashindano. Huenda walitaka Messi aendelee kubaki kwenye mbio za ubingwa,” alisema kocha wa Misri, Hossam Hassan, baada ya mchezo.

Kilichowakasirisha zaidi Wamisri ni uamuzi wa kufuta bao la kipindi cha pili lililofungwa na Mostafa Zico walipokuwa wanaongoza kwa bao 1-0. Bao hilo lilikataliwa baada ya kiungo Marwan Attia kuonekana kumkanyaga Lisandro Martínez mwanzoni mwa shambulizi lililozaa bao hilo.

Aidha, Misri walisisitiza kuwa Mohamed Salah alifanyiwa madhambi kwa namna inayofanana ndani ya eneo la hatari la Argentina sekunde chache kabla ya mabingwa hao watetezi kuanzisha shambulizi lililozaa bao la ushindi. Hata hivyo, mwamuzi hakutoa faulo wala VAR haikuingilia kati.

Katika matukio yote mawili, nafasi na matumizi ya VAR vilikuwa kiini cha mjadala mkali kuhusu usahihi wa maamuzi ya waamuzi katika mechi hiyo.

VAR ni nini, na inafanyaje kazi?

.

Chanzo cha picha, Reuters

Mfumo wa Video Assistant Referee (VAR) ulianzishwa rasmi na shirikisho la soka duniani FIFA mwaka 2018. Rais wa FIFA, Gianni Infantino, aliuelezea kama teknolojia inayolenga kuwasaidia waamuzi kufanya maamuzi bora zaidi.

Kwa ufupi, VAR ni matumizi ya teknolojia ya video kusaidia timu ya waamuzi wa uwanjani pale ambapo hawakuona tukio fulani au hawakuweza kuliona vizuri, na hivyo kufanya kosa la wazi katika uamuzi muhimu wa mechi.

Teknolojia hii humwezesha mwamuzi wa kati kutazama marudio ya tukio kutoka katika pembe mbalimbali za kamera ili kubaini kama yeye au timu yake ya waamuzi walifanya makosa wakati wa kutoa uamuzi wa awali.

Kwa mujibu wa FIFA, mfumo wa VAR unatumika katika zaidi ya mashindano 300 ya soka duniani.

Timu ya waamuzi wa VAR huchambua picha za video wakiwa katika vyumba maalumu vya uendeshaji wa video (Video Operation Rooms – VOR) vilivyo mbali na uwanja wa mechi. Katika Kombe la Dunia la FIFA 2026, waamuzi hao walikuwa wakifanya kazi kutoka kituo cha utangazaji katika jiji la Dallas, Marekani.

Iwapo waamuzi wa VAR watabaini kuwa kuna tukio linalohitaji kuchunguzwa zaidi, wanaweza kumshauri mwamuzi wa kati kwenda kutazama marudio ya tukio kwenye skrini maalumu iliyopo pembeni mwa uwanja, eneo linalojulikana kama Referee Review Area (RRA)

Baada ya kupitia video hiyo, mwamuzi wa uwanjani ndiye anayefanya uamuzi wa mwisho, ikiwa ni pamoja na kubaki na uamuzi wa awali au kuubadilisha kulingana na ushahidi wa video.

Je, VAR inaweza kutumika kwa kila aina ya tukio?

.

Chanzo cha picha, Reuters

Kabla ya mashindano ya Kombe la Dunia 2026, mfumo wa VAR uliweza kutumika katika hali nne pekee, mabao, maamuzi ya penalti, matukio ya kadi nyekundu na makosa ya kumtambua mchezaji.

Hali ya tano, ambayo FIFA inaielezea kama “mikwaju ya kona iliyotolewa kimakosa waziwazi”, imeongezwa kwenye orodha hiyo, na sasa VAR pia hutumika kukagua kadi ya pili ya njano iliyotolewa kimakosa na kusababisha kadi nyekundu.

VAR haina jukumu la kubaini kama mpira umevuka mstari wa goli au la. Hilo hukaguliwa na mfumo mwingine unaotumia chip iliyowekwa ndani ya mipira ya mechi, ambayo hutuma taarifa moja kwa moja kwa waamuzi kupitia saa mahiri (smartwatch).

VAR imetumika kwa muda gani katika Kombe la Dunia, na je, hubadili maamuzi?

.

Chanzo cha picha, Reuters

Mfumo wa VAR ulitumika kwa mara ya kwanza katika Kombe la Dunia la FIFA nchini Urusi mwaka 2018, ambapo uliingilia kati mara 20 katika mechi 64.

VAR ilibadili maamuzi 17 ya waamuzi, ikiwemo uamuzi muhimu katika mechi ya fainali. Ufaransa na Croatia zilikuwa zimetoshana kwa mabao 1-1 wakati mfumo huo ulipomfanya mwamuzi kubadili uamuzi wake wa awali wa kutoa mpira wa adhabu wa moja kwa moja nje ya eneo la penalti na badala yake kutoa penalti.

Miaka minne baadaye, katika Kombe la Dunia nchini Qatar, VAR iliingilia kati mara 27. Kila mara mwamuzi alipoelekezwa kwenda kutazama marudio ya tukio kwenye skrini iliyokuwa pembeni mwa uwanja, alibadili uamuzi wake isipokuwa katika matukio mawili pekee.

Vipi kuhusu michuano ya sasa?

.

Chanzo cha picha, Reuters

Kwa kuwa mashindano ya sasa ya Kombe la Dunia bado yanaendelea, bado hakuna takwimu kamili kuhusu matumizi ya VAR. Hata hivyo, uchambuzi wa Dale Johnson, mwandishi wa BBC Sport anayeshughulikia masuala ya soka na mtaalamu wa VAR, ulibaini kuwa mwamuzi aliitwa kwenda kutazama marudio ya video kwenye skrini ya pembeni mwa uwanja mara 23 katika mechi 96 zilizochezwa hadi sasa kwenye Kombe hili la Dunia lililopanuliwa (lenye jumla ya mechi 104). Hiyo ni idadi ndogo ya matukio kwa kila mechi ikilinganishwa na Kombe la Dunia lililopita.

Kati ya matukio hayo, ni uingiliaji kati mmoja tu wa VAR ambao haukusababisha mwamuzi kubadili uamuzi wake wa awali.

“Wiki iliyopita tu, Pierluigi Collina, mkuu wa waamuzi wa FIFA, alisisitiza moja ya vigezo muhimu alivyowapa waamuzi wake,” anaeleza Johnson.

“Waamuzi wameelekezwa kuruhusu miguso ya kawaida ya mchezo wa soka ili kuongeza kasi ya mchezo.”

Kutokana na mwongozo huo, Johnson anaongeza kuwa Kombe la Dunia la 2026 pia limeshuhudia idadi ndogo ya faulo zinazochezewa kwa kila mechi, wastani wa 22.6, ikilinganishwa na wastani wa 25 katika Kombe la Dunia la 2022 na 27 katika la 2018.

Johnson anasema uamuzi wa VAR kulifuta bao la Misri ulikuwa “haukuwa na uthabiti” ukilinganishwa na namna mechi za mashindano haya zilivyokuwa zimechezeshwa hadi wakati huo.

“Ikiwa unaruhusu aina hizi za changamoto uwanjani, basi unapaswa kufanya vivyo hivyo kupitia VAR.”

“Nafikiri matumizi ya VAR yamekuwa na ukosefu mkubwa wa uthabiti na imekuwa vigumu zaidi kutabiri ni maamuzi gani VAR itaingilia,” anahitimisha.

Hata hivyo, Johnson hakuona tukio lililomhusu Mohamed Salah kuwa la utata mkubwa.

“Salah alikuwa ndani ya eneo la penalti, hivyo VAR ilikuwa ikitathmini uwezekano wa kutolewa kwa penalti, jambo ambalo linahitaji kiwango cha juu zaidi cha ushahidi ili kuthibitisha kuwa kulikuwa na faulo.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *