Chanzo cha picha, ALEXEY NIKOLSKY/SPUTNIK/AFP
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 5
Idadi ya mabilionea nchini Urusi ilifikia kiwango cha juu zaidi kuwahi kutokea wakati wa vita dhidi ya Ukraine.
Hata hivyo, katika kipindi cha miaka 25 chini ya utawala wa Rais Vladimir Putin, matajiri na watu wenye ushawishi mkubwa nchini humo wanaojulikana kama oligarchs wamepoteza kabisa ushawishi wao wa kisiasa.
Hali hii yote imekuwa ya manufaa kwa rais wa Urusi.
Vikwazo taifa hilo imewekewa na nchi za Magharibi vimeshindwa kuwafanya matajiri hao wawe wapinzani wa Putin, huku sera ya Putin ya kutoa zawadi kwa wanaomuunga mkono na kuwaadhibu wanaompinga imewafanya wengi wao kusalia kimya na kumuunga mkono.
Aliyekuwa bilionea na mfanyabiashara wa benki, Oleg Tinkov, anafahamu vizuri jinsi adhabu hizo zinavyofanya kazi.
Siku moja baada ya kuikosoa vita hiyo kwenye chapisho la Instagram na kuviita “vita vya kichaa,” viongozi wa benki yake ya Tinkoff walipigiwa simu na Ikulu ya Kremlin.
Viongozi wa benki hiyo walitishiwa kuwa benki hiyo, ambayo wakati huo ilikuwa ya pili kwa ukubwa nchini Urusi, ingetaifishwa kama haingejitenga na kukata uhusiano wote walionao na mwanzilishi wake.
“Hatukuwa na nafasi ya kujadiliana kuhusu bei,” Tinkov aliiambia The New York Times. “Ilikuwa kama kutekwa nyara unalazimika kukubali chochote unachoambiwa. Hatukuweza kujadiliana.”
Ndani ya wiki moja, kampuni inayohusishwa na Vladimir Potanin ambaye kwa sasa ni mfanyabiashara wa tano kwa utajiri nchini Urusi, ambaye kampuni zake huzalisha nikeli inayotumika kutengeneza injini za ndege za kivita, ilitangaza kuwa ingenunua benki hiyo. Kwa mujibu wa Tinkov, benki hiyo iliuzwa kwa asilimia 3 tu ya thamani yake halisi.
Hatimaye, Tinkov alipoteza karibu dola bilioni 9 za Marekani za utajiri wake na akaondoka nchini Urusi.
Chanzo cha picha, Chris Graythen/Getty Images
Hali ilivyo sasa ni tofauti kabisa na ilivyokuwa kabla ya Vladimir Putin kuwa rais.
Katika miaka ya awali baada ya kuvunjika kwa Umoja wa Kisovieti, baadhi ya Warusi walipata utajiri mkubwa kwa kuchukua umiliki wa makampuni makubwa ambayo hapo awali yalikuwa yanamilikiwa na serikali, kwa kutumia fursa zilizotokana na mfumo mpya wa uchumi wa kibepari uliokuwa unaanza nchini humo.
Utajiri wao wa ghafla uliwapa ushawishi na nguvu kubwa wakati ambapo Urusi ilikuwa inapitia kipindi cha misukosuko ya kisiasa.
Watu hao wakajulikana kama oligarchs au matajiri wenye ushawishi mkubwa wa kisiasa na kiuchumi.
Tajiri mwenye ushawishi mkubwa zaidi nchini Urusi, Boris Berezovsky, alidai kuwa ndiye aliyepanga na kumwezesha Putin kuwa rais mwaka wa 2000.
Miaka kadhaa baadaye, alijutia uamuzi huo na kuomba msamaha.
“Mimi sikuona mapema kwamba ndani yake kulikuwa na mtawala mwenye tamaa na mwenye kunyakua madaraka, mtu ambaye angekandamiza uhuru na kuzuia maendeleo ya Urusi,” alisema mwaka wa 2012.
Wakati Putin anachukua madaraka, matajiri hao walikuwa na ushawishi mkubwa wa kushawishi maamuzi katika ngazi za juu za uongozi wa taifa hilo.
Chini ya mwaka mmoja baada ya kutoa kauli hiyo ya kuomba msamaha, Berezovsky alipatikana amefariki dunia chini ya mazingira ya kutatanisha akiwa uhamishoni nchini Uingereza.
Kufikia wakati huo, enzi ya matajiri wenye ushawishi nchini Urusi ilikuwa pia imefikia kikomo.
Chanzo cha picha, Hulton Archive/Getty Images
Rais Vladimir Putin alipowaita watu matajiri zaidi nchini Urusi katika ikulu ya Kremlin, saa chache tu baada ya kuamuru uvamizi kamili wa Ukraine tarehe 24 Februari 2022, hawangeweza kupinga ingawa walijua kwamba utajiri wao ungeathirika sana.
“Natumai kwamba, chini ya mazingira haya mapya, tutaendelea kufanya kazi pamoja kwa ufanisi uleule au hata zaidi,” aliwaambia matajiri hao.
Mwandishi mmoja wa habari aliyekuwepo katika mkutano huo alisema kwamba mabilionea waliokusanyika walionekana, wamesononeka wakiwa na wasiwasi.
Mwanzo wa uvamizi huo ulikuwa mgumu kwa mabilionea wa Urusi, na hali iliendelea kuwa mbaya baada ya vita kuendelea.
Kwa mujibu wa jarida la Forbes, idadi ya mabilionea nchini Urusi ilishuka kutoka 117 hadi 83 katika kipindi cha mwaka mmoja hadi mwezi Aprili mwaka wa 2022. Sababu kuu zilikuwa vita, vikwazo vya kimataifa na kushuka kwa thamani ya sarafu ya Urusi .
Kwa pamoja walipoteza dola bilioni 263 za Marekani sawa na wastani wa asilimia 27 ya utajiri wa kila mmoja.
Hata hivyo, miaka iliyofuata ilionyesha kwamba kulikuwa na faida kubwa kwa wale walioshiriki katika uchumi wa vita uliojengwa na Putin.
Matumizi makubwa ya serikali kwa ajili ya vita yalichochea ukuaji wa uchumi wa Urusi kwa zaidi ya asilimia 4 kwa mwaka kati ya 2023 na 2024. Hata baadhi ya matajiri ambao hawakupata mabilioni moja kwa moja kupitia mikataba ya ulinzi walinufaika kutokana na hali hiyo.
Mwaka wa 2024, zaidi ya nusu ya mabilionea wa Urusi walikuwa wanashiriki katika kusambaza mahitaji ya jeshi au walikuwa wakinufaika kwa namna fulani kutokana na uvamizi wa Ukraine, anasema Giacomo Tognini, mwandishi wa masuala ya biashara wa jarida la Forbes.
“Bila hata kuwahesabu wale ambao hawahusiki moja kwa moja lakini wanahitaji kuwa na uhusiano na Kremlin kwa namna moja au nyingine. Na ninafikiri ni sahihi kusema kwamba mtu yeyote anayefanya biashara nchini Urusi lazima awe na uhusiano mzuri na serikali,” aliiambia BBC.
Mwaka huu, orodha ya Forbes ilionyesha idadi kubwa zaidi kuwahi kutokea ya mabilionea kutoka Urusi wakiwa 140 kwa jumla. Utajiri wao wa pamoja ulifikia dola bilioni 580 za Marekani, ukiwa chini kwa dola bilioni 3 tu ikilinganishwa na rekodi ya juu kabisa iliyowekwa mwaka mmoja kabla ya uvamizi wa Ukraine.
Huku Putin akiwawezesha washirika wake waaminifu kupata faida, aliendelea kuwaadhibu wale waliokataa kufuata matakwa yake.
Warusi wengi bado wanakumbuka kilichompata tajiri wa mafuta, Mikhail Khodorkovsky. Aliyekuwa mtu tajiri zaidi nchini Urusi alitumikia kifungo cha miaka 10 gerezani baada ya kuanzisha shirika lililokuwa likitetea demokrasia mwaka 2001.
Chanzo cha picha, AFP
Tangu uvamizi wa Ukraine uanze, karibu matajiri wote wakubwa wa Urusi wameendelea kukaa kimya. Wale wachache waliothubutu kupinga vita hadharani walilazimika kuondoka nchini na kupoteza sehemu kubwa ya utajiri wao.
Ni wazi kwamba matajiri wakubwa wa Urusi ni muhimu katika kuendesha juhudi za vita za Vladimir Putin. Wengi wao wakiwemo wafanyabiashara 37 walioitwa Kremlin tarehe 24 Februari 2022 waliwekewa vikwazo na mataifa ya Magharibi.
Ingawa lengo la nchi za Magharibi lilikuwa kuwafanya wawe maskini na kuipinga utawala wa Kremlin, hilo halikufanikiwa. Utajiri wao umeendelea kuongezeka na hakuna upinzani wa wazi uliotokea kutoka kwa mabilionea wa Urusi.
Kuondoka kwa makampuni mengi ya kigeni baada ya uvamizi wa Ukraine kuliacha nafasi kubwa katika soko la Urusi. Nafasi hiyo ilijazwa haraka na wafanyabiashara wenye uhusiano wa karibu na Kremlin, ambao waliruhusiwa kununua biashara na mali zenye faida kubwa kwa bei za chini sana.
Kwa mujibu wa Alexandra Prokopenko wa Carnegie Russia Eurasia Center, hali hiyo imeunda “kundi jipya la watu wenye ushawishi na waaminifu kwa Kremlin.”
Anasema ustawi wao wa baadaye unategemea kuendelea kwa mvutano kati ya Urusi na nchi za Magharibi, huku hofu yao kubwa ikiwa ni kurejea kwa wamiliki wa zamani wa kampuni na mali walizonunua.
Kutokana na hilo, kulizuka mabilionea wapya 11 nchini Urusi ndani ya mwaka wa 2024 pekee, kulingana na Giacomo Tognini wa jarida la Forbes.
Kwa ujumla, vita pamoja na vikwazo vya Magharibi havijadhoofisha udhibiti wa Vladimir Putin juu ya watu wenye ushawishi mkubwa nchini Urusi. Badala yake, kwa namna fulani, vimemsaidia kuimarisha mamlaka yake na kuhakikisha kwamba watu hao wanaendelea kuwa waaminifu kwake.