
Khatibu wa Sala ya Ijumaa ya leo katika mji wa Tehran amesisitiza kuwa hati ya makubaliano kati ya Iran na Marekani haikuandaliwa kwa msingi wa kuuamini uongozi wa Marekani na kueleza kuwa: Mfumo wa makubaliano hayo ni ‘ahadi kwa ahadi’; na tunatangaza wazi wazi kwamba Marekani hataruhusiwa kamwe kuingilia masuala ya Mlango Bahari wa Hormuz.
Akizungumza katika hotuba zake za Sala ya Ijumaa wiki hii mjini Tehran, Hujjatul Islam Wal Muslimin Sayyid Mohammad Hasssan Abutorabi- Fard ameashiria hatua ya viongozi wa Marekani ya kukiuka makubaliano kati ya Iran na nchi hiyo kuongeza kuwa: “Viongozi wa serikali ya Marekani wamekiuka utaratibu wa makubaliano hayo kupitia hatua za upande mmoja na mashambulizi ya kihalifu, na wamefanya jinai kubwa za kivita.”
Bila shaka, mnafahamu kuwa hati hii haikuandaliwa kwa kuzingatia kuiamini serikali ya Marekani. Mfumo wa makubaliano hayo unatokana na msingi wa “ahadi kwa ahadi,” na leo hii, Iran imejizatiti na kusimama imara zaidi kuliko wakati wowote ule kulinda maslahi yake ya kitaifa pamoja na haki za washirika wake katika eneo hili.
Hujjatul Islam Abutorabi-Fardi pia amevishukuru na kuvipongeza vikosi vya ulinzi vya nchi hii yaani Jeshi la Iran na la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu IRGC kwa kulinda eneo la Mlango-Bahari wa kimkakati wa Hormuz, kuhakikisha usalama wake kwa manufaa ya mataifa yanayoutumia, na kutoa jibu madhubuti na kali kwa vitendo vya kichokozi vya jeshi la kigaidi la Marekani.
“Tunatangaza waziwazi kwamba Marekani haitaruhusiwa kamwe kuingilia masuala ya Mlango-Bahari wa Hormuz.” Amesema Khatibu wa Sala la Ijumaa wiki hii hapa Tehran.
Akiendelea na hotuba ya Sala ya Ijumaa, Hujjatul Islam Wal Muslimin Sayyid Mohammad Hasssan Abutorabi Fard ametaja marasimu ya kumuaga Kiongozi Shahidi na familia yake na kusema:” Msafara adhimu wa kuusindikiza mwili mtukufu wa Imam Khamenei umeonyesha nguvu ya Iran ya sasa, na kuimarisha nyanja mbalimbali zinazohusiana na muqawama.
Shughuli hii ya mazishi inapasa kutambuliwa kuwa tukio adhimu na kubwa lisilo na kifani, la kipekee na la kihistoria.
Wapigania uhuru duniani kote, wapenda amani na hasa mataifa ya Iraq na Iran wamejitokeza kwa namna ya kipekee na isiyo na kifani katika hafla ya kumuaga Kiongozi Shahidi; mamilioni ya watu waliojitolea kwa ajili ya Imam Shahidi kutoka nchi mbili hizo zenye nguvu zinazoongozwa kwa imani na mfumo wa demokrasia—yaani Iran na Iraq walionyesha taswira ya mfumo mpya wa Ulimwengu wa Kiislamu; mfumo unaozingatia mtazamo wa kimaanawi wa Imam Khomeini na Imam Khamenei unaolenga ukombozi na kupinga uistikbari duniani.
Khatibu wa Sala ya Ijumaa Tehran amesisitiza kuwa Kiongozi Shahidi aliuelewa Umma na uwezo wa kipekee na aina yake wa Iran na Ulimwengu wa Kiislamu na kueleza kuwa: Ayatullah Sayyid Ali Khamenei alihamasisha uwezo wa kiakili, kisayansi, kiutamaduni na kisiasa na kuuongoza Umma wa Kiislamu katika njia ya wazi kuelekea nguvu iliyojikita katika imani na mapambano mkabala wa hatua za kujitanua.