Kamanda wa Makao Makuu ya Majeshi ya Iran maarufu kwa jina la Kamandi ya Khatamul-Anbiya (SAW) amesema wale waliohusika na mauaji ya Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, watakabiliwa na adhabu, akielezea mahudhurio makubwa ya watu katika mazishi yake kuwa ni dhihirisho lenye nguvu la imani, ukakamavu na mshikamano.

Meja Jenerali Ali Abdollahi, Mkuu Kamandi ya Majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, amesema kwamba wale waliohusika na mauaji ya Kiongozi Shahidi watakabiliwa na mkono wa haki kupitia adhabu, akiongeza kwamba mahudhurio makubwa ya watu katika mazishi yatakumbukwa zaidi katika historia kama ishara ya kudumu ya utukufu, uelewa, imani, Jihadi, na Muqawama.

Kiongozi huyo wa ngazi za juu wa majeshi ya Iran amezionya Marekani na Israel dhidi ya kutafsiri maombolezo ya umma kama ishara ya udhaifu, akisisitiza kwamba mataifa ya kibeberu yanayoongozwa na “Marekani mhalifu” na “utawala muovu wa Israel” hayapaswi kufasiri isivyo huzuni na hasira ya taifa kuwa ni udhaifu.

“Maombolezo haya matakatifu na hasira ya kudai haki vitadumu katika harakati za kulipiza kisasi dhidi ya wauaji wa Kiongozi aliyeuawa shahidi, kiongozi wa Waislamu na wapigania uhuru kote duniani, pamoja na mashahidi wa vita vya pili na vya tatu dhidi ya Iran, na hatimaye watafikishwa mbele ya sheria,” amesema Jenerali Abdollahi.

Akiyataja mazishi hayo kuwa ni tamko lenye nguvu la kisiasa na kidini, Jenerali Abdollahi amesema: “Mahudhurio yasiyo ya kawaida ya Umma wa Kiislamu yalikuwa zaidi ya shughuli ya mazishi na kuaga mwili; ilikuwa sauti kubwa ya kudai utekelezaji haki na kupinga mipango ya tawala za kibeberu duiani..”

Pia ametoa shukrani zake za dhati kwa watu wa Iran na Iraq kwa kazi yao isiyo na kifani katika kuunda onyesho kubwa la umoja kupitia mahudhurio yao ya kihistoria katika mazishi yaliyofanyika katika nchi zote mbili.

“Wana jasiri wa taifa katika Jeshi, wakimtegemea Mwenyezi Mungu na kuungwa mkono na mataifa ya Kiislamu na yanayopenda uhuru, kupitia hatua za mapinduzi, watamnyima adui usingizi; na mapema au baadaye, watalipiza kisasi kwa wale waliohusika na uhalifu huu wa kigaidi,” amesisitiza Jenerali Abdollahi.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *