
Huko Kisangani, katika mkoa wa Tshopo, wagonjwa wanne waliyothibitishwa kuambukizwa virusi vya Ebola wamerekodiwa kufuatia safari kutoka Ituri, kitovu cha mlipuko huo. Watu wawili wamefariki, na wengine wawili wanapokea matibabu. Mamlaka za afya zinaongeza ulinzi na uangalizi ili kuzuia maambukizi zaidi.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Asubuhi na mapema, hospitali ya Kisangani ilipokea miili miwili kutoka Nyanya, huko Ituri. Familia zilikuwa zimewasafirisha hadi jijini humo wakati wa usiku. Miili hiyo ilikuwa ya wanawake wawili waliokuwa wanafanya kazi katika shughuli za uchimbaji madini.
Mmoja wao alikuwa mjamzito. Familia yake ilitaka afanyiwe upasuaji ili kutenganisha mtoto na mama yake kabla ya mazishi. Ni wakati huu ambapo vipimo vilithibitisha wanawake wote wawili walikuwa wameambukizwa virusi vya Ebola.
Wagonjwa wengine wawili waligunduliwa baadaye huko Kisangani. Wa tatu alikuwa mgonjwa ambaye alikimbia baada ya kituo cha matibabu kuungua huko PK50, Ituri, yapata siku kumi mapema. Wa nne alikuwa afisa wa polisi aliyeambukizwa virusi hivyo huko Nia-Nia kabla ya kufika jijini Kisangani.
Kwa jumla, Kisangani ina wagonjwa wanne waliyothibitishwa: vifo viwili na wagonjwa wawili waliowekwa karantini kwa sasa na wanapokea huduma.
Mamlaka, ikihofia ugonjwa huo unaweza kuenea katika eneo hili linalopakana na Ituri, sasa inawafuatilia watu wote ambao wametangamana na wagonjwa hawa wanne. Wizara ya Afya inaripoti kuwa imeweka mkakati wake kamili wa kukabiliana na ugonjwa huo huko Tshopo, ikiwa na ufuatiliaji, matibabu, na udhibiti ulioimarishwa katika vivuko vya mpaka ili kupunguza safari hatarishi.