
Iran na Oman zimekubaliana kuendeleza mazungumzo ya kisiasa na kiufundi kuhusu usalama wa baharini na mipango ya baadaye ya safari za meli katika Lango-Bahari la Hormuz.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baqaei amesema mapema Jumapili kwamba mazungumzo hayo, yaliyoongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje Abbas Araqchi na mwenzake wa Oman, Sayyid Badr bin Hamad Al Busaidi, mjini Muscat jana Jumamosi, yalilenga kuratibu mipango ya urambazaji na usafirishaji wa meli kati ya nchi hizo mbili kama nchi za pwani mwa Lango-Bahari la Hormuz.
Amesema, jumbe za kisheria na kiufundi za pande zote mbili pia zimeshiriki katika mazungumzo, ambayo yameshughulikia usalama wa baharini sambamba na haki za mamlaka ya nchi mbili za pwani mwa Hormuz, sheria ya kimataifa inayotumika na Kifungu cha 5 cha Mkataba wa Maelewano wa Islamabad (MoU).
Baqaei amesisitiza kwamba mfumo wowote wa baadaye unaosimamia urambazaji na safari za meli kupitia Lango-Bahari la Hormuz lazima uandaliwe kupitia mashauriano kati ya Iran na Oman kwa kuzingatia athari za kiusalama za uchokozi wa hivi karibuni wa Marekani na Israel dhidi ya Iran.
Pia amesema wawakilishi wa Qatar wameshiriki katika sehemu ya mazungumzo hayo, suala linaloonyesha nafasi ya Doha katika kuwezesha mazungumzo ya hivi karibuni kati ya Tehran na Washington.
Araqchi alikuwa Muscat jana Jumamosi kwa ajili ya mazungumzo na maafisa wa ngazi za juu wa Oman kuhusu Lango-Bahari la Hormuz, uhusiano wa pande mbili na matukio ya kikanda.