
Mazishi makubwa na ya kuvutia ya Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Seyyed Ali Khamenei, halikuwa tukio tu la maombolezo; bali lilibadilika haraka na kuwa moja ya matukio muhimu zaidi yaliyozingatiwa na vyombo vya habari na wanasiasa duniani, kieneo na kimataifa.
Kiwango cha upashaji habari, uwepo wa vyombo vingi vya habari vya kigeni mjini Tehran na aina mbalimbali za simulizi zilizochapishwa kuhusu mazishi haya vilionyesha kuwa tukio hilo lilivuka mipaka ya habari na kuwa tukio muhimu kimataifa.
Kinachopasa kuzingatiwa zaidi ni kwamba licha ya kuwa vyombo mbalimbali vya habari viliakisi mazishi hayo kwa mbinu na malengo tofauti ya kisiasa, lakini hatimaye vyote vilisisitiza hali halisi kadhaa za ukweli wa mambo: Uwepo mkubwa wa umati wa watu, mpangilio wa hali ya juu wa mazishi, umuhimu wa kikanda na kimataifa wa tukio lenyewe, na matokeo yake kwa mustakabali wa Asia Magharibi. Hali hizi ziligeuza mazishi haya kuwa moja ya matukio machache ambapo hata vyombo vya habari pinzani vililazimika kukubali ukubwa wa kuvutia wa mazishi hayo.
Katika miaka ya hivi karibuni, vyombo vya habari vya Magharibi mara nyingi vimesimulia matukio ya Iran kwa kuchochea migogoro ya ndani, maandamano ya kijamii na mashinikizo ya kiuchumi, lakini mara hii vimekabiliwa na tukio ambalo halingeweza kupuuzwa. Uwepo mkubwa wa mamilioni ya watu katika mitaa ya Tehran ulivilazimisha vyombo hivyo kuzoea hali halisi ya mambo.
Baadhi ya vyombo vya habari, kama vile The Guardian, viliashiria umati mkubwa katika mazishi hayo na kusema ni mfano wa wazi wa uwezo wa Iran wa kuandaa mikusanyiko mikubwa ya mamilioni ya watu. Reuters, ilitathmini ushiriki huo mkubwa kama ishara ya mshikamano wa ndani ya Iran baada ya vita vya karibuni na kuliona suala hili kama mafanikio makubwa kwa Iran katika mazungumzo yake na Marekani. Agence France-Presse, Associated Press, Euronews, France24, na vyombo vingine vya habari vya Magharibi kila kimoja kiliakisi mazishi hayo kwa mtazamo tofauti, lakini vyote havikuweza kufumbia macho mahudhurio ya mamilioni ya watu na umuhimu wa kisiasa wa tukio hili. Kwa kweli, propaganda za eti Jamhuri ya Kiislamu imetengwa kimataifa na kutokuwa na uungaji mkono wa raia wake haikuweza kufanya kazi tena hapa.
Katika ulimwengu wa Kiarabu, vyombo mashuhuri vya habari vikiongozwa na Al Jazeera, Al Mayadeen, Al Arabi, Al Ahad, na Al Masirah viliangazia uwepo mkubwa wa watu, umuhimu wa kikanda wa mazishi na uhusiano wake na matukio ya baada ya vita vya karibuni. Hata vyombo vya habari vyenye uhasama na Iran havikuweza kupuuza taathira kubwa za tukio hili na kulifanya kuwa moja ya habari muhimu zaidi katika ulimwengu wa Kiarabu. Vilisema mazishi haya hayakuwa mwisho wa maisha ya mtu mwenye hadhi ya kisiasa, bali yalikuwa hatua muhimu inayoamua mustakabali wa milinganyo ya nguvu katika eneo.
Vyombo vya habari vya Russia navyo vilichunguza tukio hilo kwa mtazamo wa kijiopolitiki. Mashirika ya RIA Novosti, TASS, na Sputnik yalizingatia zaidi wingi wa watu waliojitokeza na ishara za ustahimilivu na mshikamano wa kitaifa, huku yakiyachukulia mazishi hayo kuwa ishara ya uthabiti wa mfumo wa kisiasa nchini Iran.
Kwa ufupi ni kwamba tukio hili kubwa kieneo na kimataifa linaweza kufupishwa katika nukta kadhaa: Kwanza, katika ngazi ya vyombo vya habari, ambapo mazishi haya yameashiria pengo kubwa lililopo kati ya ukweli wa mambo na simulizi za kipropaganda zinazoenezwa ulimwengunu kuhusu Iran. Vyombo vya habari ambavyo kwa miaka mingi vimekuwa vikiwasilisha taswira potofu ya kutengwa Iran hatimaye vimelazimika kuzungumzia uwepo mkubwa wa watu katika mazishi ya kiongozi wao na umuhimu wake wa kisiasa.
Pili, katika ngazi ya ndani, sherehe hii imekuwa onyesho muhimu la mtaji wa kijamii na mshikamano wa kitaifa kwa jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Tatu, katika ngazi ya kikanda, mazishi haya yamebeba ujumbe wa wazi kuhusu wahusika halisi katika matukio ya Asia Magharibi. Yamethibitisha wazi pia kuwa muundo wa madaraka katika Jamhuri ya Kiislamu unategemea taasisi na kushirikishwa wananchi katika uendeshaji wa nchi na sio watu binafsi, hivyo kuondoka kwa mtu mmoja hakumaanishi kuwepo kwa ombwe la madaraka nchini.