Canada. Japo halifurahishi, ni jambo la kawaida kuona au kusikia wanandoa wakitendeana. Hutofautiana, huchukiana, husuluhishana na baya zaidi, huumizana kwa kutenzana. 

Hata hivyo, ni jambo jema wanandoa wanapotendeana kwa haki katika baadhi au nyanja zote za maisha yao kiasi cha kuridhiana, kuridhishana, na kuendelea kufaidi ndoa yao kama inavyostahili. Hapa hakuna miujiza wala mazingaombwe. Ni suala la kuelewa wajibu wa kila mmoja na kuchagua kusuka badala ya kunyoa ili nawe usukwe badala ya kunyolewa.

Leo tutazungumzia kutendeana kwa maana ya kutenzana. Kuna tofauti kubwa kati ya dhana hizi mbili. Kutendeana ni kufanyiana mambo, yawe mazuri au mabaya. Kutenzana, kwa upande mwingine, ni kuumizana. Unapomtenda vibaya mwenzako, unamchukiza, unamkosesha amani, unamhujumu, unamhukumu, na hata kumdhulumu.

 Huko ndiko kutenzana. Kuhusu kutendeana kwa maana chanya, yaani kufanyiana mema na haki, tumeshakugusia hapo juu.

Tukirejea kwenye hoja kuu ya makala hii, yaani kutendeana haki, tuseme wazi kuwa hili ndilo hitajio na dhamira kuu ya ndoa, ingawa haliwezekani bila kuwepo upendo wa kweli. 

Kwa kuwa mzizi wa ndoa ni kupendana, hatutajikita sana kwenye suala hilo, kwa sababu ni msingi unaopaswa kuwapo kabla ya mengine yote, hata kama kadri muda unavyopita hisia na mazingira hubadilika.

Wajibu wa kwanza

Kwa nini kutendeana haki si hisani bali ni wajibu? Kwanza, hakuna aliyewalazimisha kupendana wala kuoana. 

Hivyo, ikiwa mlikuwa waaminifu kwa malengo yenu, nia zenu, na viapo mlivyoweka, basi kutotendeana haki kunafuta maana halisi ya ndoa. 

Kama ndoa ipo lakini haki haipo, basi ipo kwa jina tu, si kwa maana yake kamili.

Mlitafutana, mkapendana, mkaamua kuishi pamoja, mkaapishana, na hatimaye mkafunga ndoa. Je, kwa nini mlifanya yote hayo? Jibu ni rahisi. 

Kila mmoja alikuwa akitafuta kile alichokikosa kwake lakini alichoamini kingepatikana kwa mwenzake. Kwa hiyo, kutendeana haki si chaguo, wala si hisani. 

Ni hitaji muhimu linaloifanya ndoa iwe na maana na kudumu.Sisi waandishi ni wanandoa ambao tumedumu kwenye ndoa kwa takribani miaka 30.

 Tunaijua ndoa kwa ndani na kwa nje. Tumeiona katika mapana na marefu yake. Tunazijua raha zake na karaha zake. 

Hivyo, tunapoandika haya hatusimulii nadharia tulizosoma vitabuni pekee, bali tunachanganya uzoefu wetu binafsi na utafiti tuliofanya kuhusu maisha ya ndoa.

Kuna msemo maarufu wa Kifaransa unaosema:  ‘l’essence du droit est l’essence du devoir, yaani, kiini cha haki ni wajibu. 

Kwa maneno mengine, bila kutimiza wajibu hakuna haki ya kudai. Kwa lugha yetu ya Kiswahili,  tunaweza kusema mikono miwili hunawishana, au nikune nikukune. 

Ndoa ni ushirika wa watu wawili wanaowajibika kwa kila mmoja ili kila mmoja apate haki yake.

Nasi tuna msemo wetu. Kwetu, ndoa ni biashara ya watu wawili wenye malengo yanayofanana na waliokubaliana kuyaendea pamoja. Kama kweli mnapendana, mtatendeana haki. 

Hapa haki si hisani wala ombi; ni wajibu. Katika ndoa, haki huenda sambamba na upendo, heshima, na uwajibikaji.

Kwa mfano, mume anaweza kutaka mke amtii kwa madai kwamba hiyo ni haki yake na wajibu wa mke. 

Lakini je, inawezekana kutarajia utiifu bila yeye mwenyewe kuwa tayari kumheshimu na kumsikiliza mke wake? Kumbuka, mwenzako si roboti asiye na hiari, hisia, au uwezo wa kuhoji. 

Kwa nini utake mtu mwenye akili kama wewe, au hata zaidi yako, akutii ilhali wewe huko tayari kumjali na kumheshimu?

Je, inawezekana kutiiwa bila kumtii anayekutii katika maisha ya kawaida? Hilo linaweza kutokea kwenye utumwa, ukoloni, au tawala za kidikteta, lakini si katika jamii ya watu wastaarabu wanaojenga uhusiano kwa hiari. 

Kama wanandoa wanavyokubaliana katika mambo mengine ya maisha yao, ndivyo wanavyopaswa kukubaliana pia katika kutendeana haki.

Katika maisha yetu ya ndoa tunayo kanuni moja rahisi lakini yenye nguvu. Mara nyingi huulizana: Kama ungekuwa mimi, ungefanyaje? Au, ungependa nikufanyie nini kama ungekuwa katika nafasi yangu? 

Hapo ndipo tunapopata majibu ya haki. Kwa maana nyingine, kila unachomfanyia mwenzako, kwa namna fulani unajifanyia wewe mwenyewe kupitia kwake.

Bila kuficha wala kufumba, katika tendo la ndoa, ambalo tumeliita kwa heshima “chakula cha usiku”, nani humtegea mwenzake? Nani hutoa bila kutarajia kupokea, au hupokea bila kutarajia kutoa? 

Ukitaka kujibu swali hili kwa usahihi, jiulize: kama mwenzako asingekuwapo kwa sababu yoyote ile, hali ingekuwaje? Ukweli ni kwamba utoacho ndicho utakachopokea kutoka kwa mwenzako. Zaidi ya hapo, kila unachomfanyia mwenzako hukurudia kwa namna moja au nyingine.

Waingereza wana msemo unaosema kwamba ukitenda wema, wema utakurudia; na ukitenda ubaya, nao utakurudia. Hivyo basi, ukimpenda mwenzako, kwa hakika unajipenda mwenyewe. Ukimchukia, unajichukia pia. Vivyo hivyo, ukimnyima haki au ukamdhulumu, kwa namna fulani unajinyima haki na kujidhulumu mwenyewe.

 Je, kuna faida gani ya kufanya hivyo ilhali unajua mwisho wa yote mtabaki mmeumizana nyote wawili?

Tumalizie kwa kurejea kwenye suala la kuishi pamoja na kupeana “chakula cha usiku”. Lazima wanandoa wafahamu kuwa kupata na kutoa ni sehemu mbili zinazokamilishana. 

Hakuna anayepata bila mwenzake kutoa, na hakuna anayetoa bila kutarajia kupokea kwa namna fulani. Kama ilivyo kwa chakula chochote, maandalizi ni muhimu kabla ya kula. Vivyo hivyo katika tendo la ndoa. 

Kama hujamlainisha mwenzako kihisia na kimwili, huenda usifanikiwe au ukafanikiwa kwa maumivu badala ya furaha. 

Vivyo hivyo, kama mwenzako hajakutayarisha, mnaweza kushiriki tendo hilo lakini likakosa ladha na kuridhisha. 

Tunadhani tunaeleweka. Kwa nini msijiandae na kulainishana ili wote wawili mpate kile mnachokihitaji?

Kwa ujumla, kila mnachofanyiana kwa hiari, kwa heshima, na kwa makubaliano ni haki yenu nyote wawili. Vivyo hivyo, kila mnachonyimana bila sababu ya msingi ni dhuluma dhidi ya mwenzenu na, hatimaye, dhidi yenu wenyewe. Ndoa yenye afya hujengwa juu ya kutendeana haki, si kutarajia hisani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *