
Dar es Salaam. Wazazi wengi huamini mtoto atasoma vizuri endapo atasukumwa kila wakati, atawekewa ratiba kali au ataadhibiwa kila anapofanya vibaya.
Hata hivyo, wataalamu wa malezi wanasema nidhamu ya kweli ya kujifunza kwa mtoto mara zote huwa haijengwi kwa hofu, bali kwa kumlea mtoto ajitawale na kuona thamani ya elimu mwenyewe.
Katika ulimwengu wa sasa, mafanikio ya mtoto hayategemei akili pekee. Yanategemea pia uwezo wa kujisimamia, kupanga muda, kuwajibika na kuendelea kujifunza hata pale ambapo hakuna anayemsimamia.
Hii ndiyo inayojulikana kama ‘learning discipline’ kwa maana ya nidhamu ya kujifunza.
Mtaalamu mmoja wa saikolojia ya maendeleo wa Chuo Kikuu cha Stanford, Profesa Carol Dweck katika moja ya maandishi yake, anasema watoto wanaofundishwa kuamini kuwa uwezo unaweza kukua kupitia juhudi na mazoezi, huwa na motisha ya kujifunza kuliko wanaolelewa wakiamini mafanikio yanatokana na kipaji pekee.
Mtaalamu huyu anawaelekeza wazazi kwamba wanapaswa kutambua kuwa mtoto anayesifiwa kwa juhudi, uvumilivu na namna alivyotatua changamoto, humjengea ari ya kujifunza kwa muda mrefu kuliko anayesifiwa kwa kusema tu ni mwerevu.
Hii ina maana kuwa mzazi anapompongeza mtoto kwa bidii aliyoonyesha badala ya matokeo pekee, humfundisha kuwa kujifunza ni mchakato unaohitaji jitihada.
Kwa maana hiyo, wazazi wanapaswa kutambua kuwa nidhamu ya mtoto kujifunza, mara zote huanzia nyumbani.
Mtoto anayeshuhudia wazazi wake wakisoma vitabu, magazeti au kujifunza ujuzi mpya, huona kujifunza kama sehemu ya maisha ya kawaida. Kinyume chake, mzazi anayesisitiza mtoto asome huku yeye mwenyewe hajengi utamaduni wa kujifunza akiwa nyumbani, hutuma ujumbe unaochanganya.
Mazungumzo ya kila siku kuhusu kile mtoto alichojifunza shuleni, yanaweza kuwa na mchango mkubwa kuliko kumhoji kwa ukali kuhusu alama alizopata.
Wataalamu pia wanaonya dhidi ya tabia ya wazazi kufanya kazi za watoto wao ili wapate alama nzuri. Ingawa inaweza kuonekana kama msaada, lakini humnyima mtoto nafasi ya kujifunza kuwajibika na kutatua changamoto zake zinazomkabili.
Badala yake, mzazi anashauriwa, amwelekeze mtoto namna ya kupanga kazi zake, kutafuta taarifa na kufikiri, kwa kufanya hivyo, humjengea uwezo wa kujitegemea ambao utamnufaisha hata ukubwani.
Aidha, mzazi hapaswi kuwa mkali kiasi cha kumfanya mtoto asome kwa hofu, wala asiwe mlegevu kiasi cha kumwacha afanye kila anachotaka. Kinachohitajika ni uwiano.
Teknolojia nayo imeongeza changamoto mpya. Simu za mkononi, michezo ya mtandaoni na mitandao ya kijamii huvuta umakini wa watoto kwa urahisi.
Hali hii inahitaji wazazi kuweka utaratibu unaoeleweka kuhusu muda wa matumizi ya vifaa vya kidijitali bila kutumia vitisho kila wakati.
Mtoto anaposhirikishwa katika kuweka ratiba ya masomo na mapumziko, hujifunza kuwajibika kwa makubaliano aliyoshiriki kuyafanya.
Jambo lingine muhimu ni kumruhusu mtoto afanye makosa. Wapo mtakaoshangaa kwa nini ninasema hivyo.
Lakini ukweli ni kwamba, wapo wazazi wengi huingiwa na hofu mtoto anaposhindwa mtihani au kufanya vibaya darasani. Lakini kushindwa kunaweza kuwa sehemu ya kujifunza endapo kutatumika kama fursa ya kutafuta kilichosababisha matokeo hayo na namna ya kuboresha.
Lengo lisiwe kumlea mtoto anayepata alama 100 kila mara, bali anayejifunza kutokana na makosa na haogopi kujaribu tena.
Aidha, kila mtoto ana namna yake ya kujifunza. Wapo wanaojifunza kwa kusoma, wengine kwa kusikiliza, kuandika au kufanya vitendo. Kumlinganisha mtoto na ndugu yake au mwanafunzi mwingine, kunaweza kumpunguzia ari yake ya kujifunza badala ya kuiongeza.
Mzazi anapaswa kutambua nguvu za mtoto wake na kumsaidia kuziendeleza huku akimsaidia kuboresha maeneo yenye udhaifu.
Mwisho wa yote, mzazi asijione kuwa kazi yake ni kumsimamia mtoto kila dakika. Lengo la malezi bora ni kumfanya mtoto afike mahali aone kwamba anaweza kujisimamia mwenyewe.
Atakapofikia hatua ya kufungua kitabu bila kukumbushwa, kupanga muda wake wa masomo na kutafuta majibu ya maswali yake kwa hiari, ndipo mzazi atakuwa ametimiza jukumu kubwa la malezi.