KOCHA wa makipa, Fernando Pereira, ameaga ndani ya klabu ya Yanga baada ya kumaliza safari yake akiwa sehemu ya benchi la ufundi lililoiongoza timu hiyo kutwaa ubingwa wa tano mfululizo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Kocha huyo raia wa Angola, ametoa ujumbe wa shukrani kupitia akaunti yake rasmi ya Instagram, akieleza furaha na fahari yake kwa kuwa sehemu ya mafanikio ya Yanga, akisisitiza kuwa ubingwa huo umetokana na kazi ya pamoja ya kila mtu ndani ya klabu.
“Ni kwa furaha na fahari kubwa kusherehekea ubingwa wa tano mfululizo. Ushindi huu hauonyeshi tu vipaji na kujituma kwa wachezaji wetu, bali pia kazi kubwa na mapenzi ya kila mmoja aliyeshiriki katika safari hii,” ameandika Pereira.
Pereira aliwashukuru wachezaji kwa kujituma kwao katika msimu mzima, akisema walionyesha nidhamu, kujitoa na ari ya ushindani iliyoiwezesha Yanga kuendelea kutawala soka la Tanzania.
Mbali na wachezaji, amewapongeza viongozi wa benchi la ufundi na wafanyakazi wote wa klabu hiyo, akieleza kuwa walifanya kazi kwa weledi mkubwa na kuhakikisha mazingira yanakuwa rafiki kwa timu kupata mafanikio.
“Nawashukuru kwa dhati kila mmoja wa benchi la ufundi. Kujituma kwenu na taaluma yenu vilikuwa msingi wa mafanikio haya. Mlikuwa tayari kila wakati kuwasaidia na kuwaongoza wachezaji wetu,” ameandika.
Kocha huyo pia amewapa shukrani wadhamini wa klabu kwa kuendelea kuiunga mkono Yanga katika safari yake ya mafanikio, akisema mchango wao ulikuwa muhimu katika kufanikisha malengo ya timu.
Hakuwasahau mashabiki wa Yanga ambao amewataja kuwa ndiyo nguvu kubwa ya timu, akisema mapenzi yao kwa klabu yamekuwa chachu ya mafanikio yaliyopatikana.
Pereira amesema anaondoka akiwa na kumbukumbu nyingi nzuri huku akijivunia kuwa sehemu ya kikosi kilichomaliza msimu kwa kutwaa ubingwa wa ligi sambamba na kuwa na safu bora ya ushambuliaji na ulinzi.
“Hatukusherehekea tu ubingwa, bali pia tulimaliza tukiwa na safu bora ya ulinzi na ushambuliaji. Hii ni uthibitisho wa kazi ya pamoja na kujitoa kwa kila mmoja ndani ya klabu,” amebainisha.
Ingawa Pereira hajaeleza sababu za kuondoka kwake wala hatua yake inayofuata, ujumbe wake umeashiria mwisho wa safari yake ndani ya Yanga baada ya kutua Oktoba 25, 2025 sambamba na kocha mkuu, Pedro Goncalves ambaye alikuwa wa kwanza kuondoka alipositishiwa mkataba Mei 6, 2026.
Kuondoka kwa Pereira kunafuatia mabadiliko yanayoendelea ndani ya benchi la ufundi la Yanga, ambapo klabu hiyo tayari imemtambulisha kocha mkuu mpya, Manqoba Mngqithi raia wa Afrika Kusini, atakayeongoza kikosi hicho kuanzia msimu ujao wa 2026-2027.