Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Ayoub Mohammed Mahmoud amesema utamaduni wa Zanzibar unaweza kuwa kichocheo cha ukuaji wa uchumi endapo utaendelezwa na kuwekewa mazingira ya kugeuzwa kuwa bidhaa ya kibiashara.

Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Zanzibar ndani ya Maonyesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba),  Waziri huyo amesema urithi wa Zanzibar katika mila, mavazi, muziki, vyakula na lugha ni sehemu ya fursa zinazoweza kuongeza mapato kupitia utalii na biashara.

Amesema Zanzibar ina historia ya muda mrefu ya kuwa kitovu cha biashara katika ukanda wa Bahari ya Hindi, ikitokana na nafasi yake ya kimkakati, rasilimali na uwezo wa kuunganisha watu na masoko mbalimbali.

“Zanzibar ina historia ya muda mrefu katika biashara na imekuwa kiungo muhimu cha biashara katika ukanda wa Bahari ya Hindi kwa karne nyingi. Historia hiyo imejengwa kupitia bidii ya wananchi wake, rasilimali zake, eneo lake la kimkakati na uwezo wake wa kuunganisha watu na masoko,” amesema.

Amesema pamoja na udogo wa eneo la Zanzibar, ubora wa bidhaa na huduma zake unaweza kuifanya iwe mshindani mkubwa katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

Baadhi ya wananchi wameendelea kujitokeza kwa wingi kwenye Banda la Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), ikiwa imebaki siku Moja kumalizika kwa Maonesho ya 50 ya Biashara ya Dar es Salaam ya Kimataifa (DITF) maarufu sabasaba.. Picha na Said Pow

“Kwa ukubwa wa eneo Zanzibar ni ndogo, lakini kwa ubora wa bidhaa na huduma Zanzibar ni kubwa zaidi ya tunavyofikiria. Tuende tukashindane kwa ubora wa bidhaa, vifungashio na utoaji wa huduma,” amesema.

Ameongeza kuwa uwekezaji katika rasilimali watu ni muhimu ili kuwawezesha wazalishaji na wajasiriamali wa Zanzibar kufikia masoko mapana.

Amesema Siku ya Zanzibar katika maonyesho hayo imekuwa jukwaa la kuonyesha utambulisho wa Mzanzibari kupitia utamaduni, bidhaa na fursa za kiuchumi zilizopo visiwani humo.

Amesema wageni wanaotembelea Zanzibar wanapaswa kupata nafasi ya kuona na kujifunza utamaduni wake kama sehemu ya uzoefu wa utalii.

“Endapo tutayaendeleza haya na kuweka kituo maalumu cha kuyaonyesha, wageni wanaokuja Zanzibar hawataondoka bila kufika kwenye kituo hicho,” amesema.

Ameonya kuwa kuna umuhimu wa kuhifadhi historia na tamaduni za zamani ili zisipotee kutokana na mabadiliko ya kizazi.

“Tusije tukasahau wale waliopita kwa kuangalia tu mambo ya kisasa. Ni vyema tukumbushane kwa kuyaweka yale na kuyaonyesha,” amesema.

Katika hatua nyingine, Waziri huyo ameitaja lugha ya Kiswahili kama moja ya fursa kubwa za kiuchumi kwa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla, akisema inaweza kusaidia kukuza ajira kupitia utalii, elimu na biashara.

Amesema Zanzibar itaendelea kushirikiana katika kukitangaza Kiswahili duniani kwa kuwa ni sehemu muhimu ya utambulisho wake.

Akizungumzia maadhimisho ya miaka 50 ya Sabasaba, amesema maonyesho hayo yamekuwa daraja la kuunganisha wafanyabiashara, wazalishaji, wabunifu na wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi.

Baadhi ya wananchi waliojitokeza kwenye Maonesho ya 50 ya Biashara ya Dar es Salaam ya Kimataifa (DITF) maarufu sabasaba wakiangalia Miche ya mazao mbalimbali inayouzwa kwenye Maonesho hayo jijini Dar es Salaam leo, Julai 12, 2026. Picha na Said Powa

Amesema ushiriki wa Zanzibar katika maonyesho hayo kwa miaka yote 50 umeiwezesha kutangaza bidhaa zake, kuonyesha ubunifu wa wananchi wake na kufungua milango ya ushirikiano wa kibiashara.

“Ukuaji wa biashara unahitaji bidhaa bora, ubunifu, viwango vinavyokubalika, vifungashio vinavyovutia na uwezo wa kufikia masoko mapana,” amesema.

Aidha, amesema kauli mbiu ya Sabasaba mwaka huu inayosisitiza fahari ya Tanzania inaonyesha namna maonyesho hayo yalivyovuka mipaka ya nchi kutokana na ushiriki wa mataifa mbalimbali.

Amesema ushiriki wa nchi zaidi ya 26 na uwepo wa viongozi kutoka mataifa jirani unaonyesha kuwa Sabasaba limekuwa jukwaa la kimataifa la biashara na uwekezaji.

Katika hatua nyingine amesema upo umuhimu wa kuwapo kwa ushirikiano kati ya Zanzibar, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sekta binafsi na wawekezaji katika kujenga uchumi imara unaoendana na Dira ya Maendeleo ya Tanzania ya mwaka 2050.

Kwa upande wake, Katibu wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar, Arif Abbas  amesema siku hii inafanyika wakati ambao Julai 28 mwaka huu Zanzibar inatarajiwa kuwa mwenyeji wa tuzo za utalii wa dunia (World Travel Award) huku Rais wa Zanzibar, Hussein Mwinyi akitarajiwa kuwa mgeni rasmi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *