Chanzo cha picha, Getty Images
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imelaani mashambulizi mapya ya Marekani na kuonya kuwa mataifa ya Ghuba yatakayoshirikiana katika kile ilichokiita “uchokozi wa kijeshi dhidi ya Iran” yatakuwa shabaha halali za vikosi vya jeshi la Iran.
Tamko hilo lilichapishwa na vyombo rasmi vya habari vya Iran Jumatatu asubuhi, Julai 13.
Katika taarifa hiyo, Iran iliishutumu Marekani kwa kukiuka makubaliano yaliyofikiwa hivi karibuni ya kusitisha vita.
“Katika muda wa siku 25 tu tangu kusainiwa kwa makubaliano ya kumaliza vita, utawala wa Marekani umekiuka wazi karibu masharti yote ya makubaliano hayo na umetenda uhalifu mkubwa wa kivita kwa kushambulia miundombinu ya usafiri ya Iran, boti za uvuvi, meli za mizigo, vituo vya hali ya hewa na miundombinu mingine,” ilisema taarifa hiyo.
Wizara hiyo pia ilisema kuwa kwa mujibu wa sheria za kimataifa, nchi jirani zina wajibu wa kuhakikisha maeneo yao hayatumiwi kutekeleza mashambulizi dhidi ya Iran.
“Nchi jirani zina wajibu chini ya sheria za kimataifa kuzuia eneo lao au miundombinu yao kutumiwa kwa uchokozi wa kijeshi dhidi ya Iran. Eneo lolote litakalotumiwa kupanga au kutekeleza mashambulizi dhidi ya Iran litachukuliwa kuwa shabaha halali ya mashambulizi ya kujihami ya vikosi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran,” taarifa hiyo iliongeza.
Wakati huo huo, mamlaka mpya inayosimamia usafiri katika Mlango wa Hormuz imesema shughuli za usafirishaji kupitia njia hiyo zimesimamishwa kutokana na mashambulizi ya kijeshi na kuongezeka kwa shughuli za kijeshi za Marekani katika maji ya Ghuba ya Uajemi.
Mamlaka hiyo ilitangaza kuwa Mlango wa Hormuz utaendelea kufungwa hadi itakapotolewa taarifa nyingine.
Soma Zaidi Hapa: