
Madaktari, wauguzi na wanaharakati wamekusanyika nje ya Chuo cha Kifalme cha Watoto na Afya ya Watoto (RCPCH) jijini London, wakitaka hatua zichukuliwe dhidi ya kukamatwa kinyume cha sheria daktari wa watoto wa Kipalestina Dkt. Hussam Abu Safiya anayeshilikiwa na utawala ghasibu wa Israel.
Madaktari na wauguzi hao wamewasilisha ombi lao wakihimiza chuo hicho kutoa wito hadharani wa kuachiliwa mara moja Dkt. Hussam Abu Safiya pamoja na wafanyakazi wengine wa afya wa Kipalestina wanaoshikiliwa katika magereza za Israel.
Waandaaji wa mkusanyiko huo wanasema Chuo cha Kifalme cha Watoto na Afya ya Mtoto, (Royal College of Pediatrics and Child Health) ambacho kinawakilisha maelfu ya wataalamu wa afya ya watoto kote nchini Uingereza na duniani, kinapaswa kutumia ushawishi wake kuwatetea madaktari wenzao wa watoto wanaofanya kazi katika maeneo yenye migogoro.
Wanasema kwamba ukimya cha taasisi zinazoongoza za matibabu unaweza kuhalalisha mashambulizi dhidi ya wafanyakazi wa huduma za afya na hospitali, hasa katika maeneo ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu.
Maandamano hayo yanakuja huku mashirika ya kimataifa yakiendelea kueleza wasiwasi wao kuhusu athari za vita vya mauaji ya kimbari vya Israel katika sekta ya afya ya Ukanda wa Gaza.
Wanaharakati wanasema kwamba wataalamu wa huduma za matibabu hawapaswi kamwe kuwa shabaha wakati wa vita na wanasisitiza kwamba jamii ya kimataifa inapaswa kuzidisha mashinikizo ili kuhakikisha wafanyakazi wa afya wanaoshikiliwa kizuizini huko Israel wanaachiwa huru.
Wafanyakazi hao wa huduma za afya wa Uingereza wanasema kampeni hiyo haihusu mtu mmoja na kwamba kukamatwa Dkt. Abu Safiya kumekuwa nembo ya hatari kubwa zaidi inayoikabili jamii ya huduma za matibabu huko Gaza.