Arusha.  Nimepata bahati ya kufanya utafiti kuhusu malezi zama za mababu zetu katika bara la Afrika, nikijikita zaidi katika nchi za Afrika ya Mashariki, na zaidi sana katika kabila langu.

Vyanzo vyangu vikuu vya habari nilizozipata vilikuwa kumbukumbu zangu za utotoni, tafakari juu ya uzoefu huo, hadithi nilizosikia utotoni, makuzi niliyopata mimi mwenyewe, malezi niliyoshuhudia dada zangu wakiyapata, maandishi ya waandishi Waafrika wenzangu, maandishi ya wageni kutoka ulaya (wamisionari na waadishi wengine), na utafiti wangu endelevu hadi wakati huu.

Ni vyema kutambua kwamba malezi ya watoto yalianza mara tu mtoto alipozaliwa, hivyo kwamba unaweza kuainisha vipindi vifuatavyo katika malezi hayo:

Malezi ya mtoto mchanga, malezi ya mtoto mdogo (infant), malezi ya mtoto (child), malezi ya mtoto wa wa kike, malezi ya mtoto wa kiume, malezi ya vijana wa kike na wa kiume, malezi ya watu wazima na malezi ya jamii nzima kwa ujumla.

 Utaratibu huu wa malezi kufuatana na umri na jinsia ya mtu upo hadi leo kwa jamii ya Kimasai kwa kiasi fulani, lakini kwa makabila mengi utaratibu huu umefifia au umepotea moja kwa moja.

Utafiti huo umenionesha kwamba watoto wa kike na wa kiume kwa ujumla,  walikuzwa pamoja kuanzia kuzaliwa hadi umri wa miaka minne au mitano.

Kuanzia umri huo watoto walipewa makuzi tofauti kufuatana na jinsi zao. Katika makala hii tutaona jinsi mtoto wa kike alivyokuzwa na katika makala yajayo tutaona makuzi ya mtoto wa kiume.

Makuzi mtoto wa kike

Lengo la malezi kwa ujumla zama hizo lilikuwa ni kumkuza mtoto ili awe na haya mawili: malezi ya kiroho yaani tabia njema iliyosimamishwa katika uadilifu thabiti, (education for life), na malezi yaliyomtayarisha mtoto aweze kujitegemea kiuchumi na hivyo kuiendeleza familia yake na jamii yake kiuchumi.(education for a living).

Hadi kufikia umri wa miaka minne watoto wa kiume na wa kike walionekana wakicheza pamoja wakati wa mapumziko, lakini kuanzia umri huo mama alianza kumpa mtoto wake wa kike malezi au makuzi tofauti na wa kiume.

Mama alikuwa kiongozi katika haya makuzi ya binti yake, na mara nyingi alishirikiana na kinamama wengine katika ukoo wao kama bibi yake na pia mashangazi wake. Hawa ndio walikuwa walimu wakuu wa binti huyu, wakiongozwa na mama yake mzazi.

Majukumu ya nyumbani

Mama alianza kumpa binti yake mafunzo katika matendo kama vile kuhakikisha nyumba na mazingira yake ni safi, na kumsaidia mama katika majukumu yake yote kwa ujumla.

Nilimuona mama yangu akimfundisha dada yangu mdogo jinsi ya kupika, na pia usafi katika mapishi na katika maandilizi ya chakula hadi kiliwe na familia.

Mama alimwelekeza bintiye mdogo ahakikishe kuna maji ya kunywa, kupikia, kufua nguo na kadhalika. Kwetu ilikuwa desturi kwamba mama awatunze ng’ombe na baba awashughulikie mbuzi na kondoo. Hivyo mama alimfundisha binti yake jinsi ya kupata majani ya ng’ombe, kuwalisha, na pia kuhakikisha usafi wa wanyama hao na mazingira yao.

Huyu binti ana umri wa miaka minne. Kwetu sisi ng’ombe, mbuzi na kondoo walilishwa bandani mwao, hawakupelekwa malishoni kama ilivyo kwa Wamasai.

Mama alitumia aina ya kisu kilichoitwa ishami kukata majani, na alimpa binti yake kishami kidogo ili naye akate majani kwa ng’ombe zao. Binti huyu alifunzwa kuchukua mbolea ya wanyama na kuisambaza shambani.
 

Upishi na kilimo

Binti huyu akifikisha umri wa miaka sita, mama yake anaanza kumfundisha upishi, hasa kwa mifano yake. Mama alielewa vizuri kwamba kufundisha kwa mifano mizuri ndio hasa njia kuu ya kumlea mtoto. Ukweli huu waliuelewa vizuri mababu zetu: njia bora kuliko zote za kumlea mtoto ni kupitia mifano mizuri.

Binti huyu akifikia umri wa miaka minane, mama yake ataanza kumpa malezi ya kina katika kilimo. Kwetu tulikuwa na mazao haya: migomba, kahawa, na mbogamboga za aina mbalimbali. Binti huyu alifunzwa mbinu zote za kilimo akajua aina ya mbegu, wakati wa kuotesha hiki au kile, kupalilia, na kuvuna. Huyu binti ana miaka minane.

Akifikisha umri wa miaka 10 hadi 12, binti huyu ni mpishi bora, mkulima mzuri, mtaalamu wa usafi wa nyumbani na mazingira yake.

Mama akienda sokoni anamchukua binti yake na huko atafunzwa kufanya biashara ndogo ndogo kama kuuza na kununua ndizi, maboga na vyakula vingine.

Uadilifu na busara

Katika shughuli hizi zote za kumlea binti yake kiuchumi, kuna malezi mengine yanayoendelea wakati wote huu sambamba na makuzi ya kiuchumi na kijamii.

Haya ni makuzi ya kiroho ambayo yanakwenda pamoja na hayo mengine. Wakiwa jikoni au shambani au sokoni, mama anakoleza masomo hayo kwa kumpa bintiye hadithi za watu waadilifu, za kinamama shujaa waliosifika katika ukoo na jamii.
 Mama humfundisha bintiye mbinu za kuwa mke bora baadaye, kuwa na uvumilivu katika ndoa, na kukua katika uadilifu kama mama wa familia.

Siku moja nilimsikia mama yangu akimweleza mdogo wangu jinsi ya kuishi na mume, jinsi ya kuongea naye wakati wa amani na wakati wa shari. Kwa kifupi mama aliwatayarisha wadogo zangu kuwa wake bora baadaye maishani mwao.

Tufanye leo

Hapo zamani malezi ya mtoto wa kike yaliongozwa na mama yake akisaidiana na bibi na mashangazi. Kati ya mama na binti palijengwa ukaribu ambao ndio ulikuwa msingi mkuu wa kumtayarisha binti yake awe mwadilifu na mchapakazi katika maisha ya wakati huo na baadaye.

Msisitizo hapa ni ule ukaribu wa mama na binti yake. Zama hizi mazingira ni tofauti lakini naona kwamba tunaweza kuwasaidia binti zetu ipasavyo ikiwa mama na binti yake watajenga ukaribu ambao juu yake malezi bora yatajengwa.

Ukaribu huo utampa nafasi mama amjenge binti yake kimaadili na kiuchumi. Pia ukaribu huo utawafanya wote wawili waweze kuongea mambo yote ya maisha kwa uwazi. Hayo niliyaona kati ya mama yangu na wadogo zangu wa kike.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *