RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameishukuru Serikali ya Sweden kwa ushirikiano wake wa muda mrefu katika kuchangia maendeleo ya Zanzibar, huku akihimiza kuimarishwa kwa ushirikiano wa kiuchumi kupitia biashara na uwekezaji.
Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo, Julai 14, 2026, alipokutana na Balozi wa Sweden nchini Tanzania, Charlotta Ozaki Macias, aliyefika Ikulu Zanzibar kwa ajili ya kumuaga baada ya kumaliza muda wake wa kazi nchini.
Katika mazungumzo hayo, Rais Dk. Mwinyi amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji ili kuvutia wawekezaji wa ndani na nje katika sekta mbalimbali za kimkakati. SOMA: Benki ya Equity zaidi kupasua anga Zanzibar

Amezitaja sekta zenye fursa kubwa za uwekezaji kuwa ni pamoja na nishati, uchumi wa buluu na kilimo cha mwani, akieleza kuwa Serikali inakaribisha makampuni ya Sweden kuwekeza, hususan katika uzalishaji wa nishati mbadala ili kuongeza uzalishaji wa umeme na kuchochea ukuaji wa uchumi. Aidha amesema Serikali imejipanga kuongeza thamani ya zao la mwani kupitia usindikaji na uzalishaji wa bidhaa mbalimbali, hatua inayotarajiwa kuongeza kipato cha wakulima na kuimarisha uchumi wa buluu.
Kwa upande wake, Balozi wa Sweden nchini Tanzania, Charlotta Ozaki Macias amempongeza Rais Dk. Mwinyi na wananchi wa Zanzibar kwa hatua zilizofikiwa katika kuimarisha maridhiano ya kisiasa kupitia Tamko la Pamoja na utiaji saini wa ajenda za utekelezaji kati ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na ACT-Wazalendo.