SERIKALI imetangaza operesheni kabambe ya kudhibiti bidhaa za magendo na biashara haramu katika mpaka wa Horohoro, Wilaya ya Mkinga mkoani Tanga, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kulinda usalama wa taifa na kuongeza ukusanyaji wa mapato ya Serikali.

Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar wakati wa ziara yake katika Kituo cha Forodha cha Horohoro, ambapo amesisitiza kuwa Serikali haitafumbia macho mtandao wowote wa uvunjifu wa sheria unaofanyika mipakani.

Balozi Omar amesema biashara ya magendo ni tishio kwa usalama wa taifa na uchumi wa nchi, akibainisha kuwa jukumu la maofisa wa forodha na vyombo vya ulinzi si kukusanya mapato pekee, bali pia kuhakikisha bidhaa hatarishi haziingizwi nchini kinyume cha sheria. “Tusipotekeleza jukumu hili ipasavyo, tutalisababishia Taifa madhara makubwa. Usalama wa taifa ni jambo ambalo hatuwezi kulifumbia macho hata kidogo,” alisema Balozi Omar. SOMA: TRA Geita yatoa onyo biashara za magendo

Ameongeza kuwa ukusanyaji wa takwimu sahihi za biashara ni nyenzo muhimu kwa Serikali katika kupanga mipango ya maendeleo, hivyo kudhibiti magendo kutasaidia kuimarisha uchumi wa taifa na kuongeza mapato ya ndani.Kwa upande wake, Afisa Mfawidhi wa Kituo cha Forodha Horohoro, Shadrack Mbonea, amesema kituo hicho kinakabiliwa na changamoto ya kukosekana kwa mashine ya kisasa ya kukagua mizigo (scanner), hali inayopunguza ufanisi wa ukaguzi wa bidhaa zinazopita mpakani.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Mkinga, Gilbert Kalima amesema miundombinu duni ya barabara katika maeneo ya mpakani imeendelea kutoa mwanya kwa wafanyabiashara wasio waaminifu kutumia njia zisizo rasmi. Amesema Serikali ya Wilaya itaendelea kushirikiana na mamlaka husika kuhakikisha njia hizo zinadhibitiwa ili kuimarisha usalama wa mipaka na kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *