SERIKALI imewataka wachezaji wa timu ya taifa ya judo kupambana kwa nguvu zote katika Michezo ya Jumuiya ya Madola ili kuiletea Tanzania medali, ikisisitiza kuwa taifa lina matarajio makubwa kwao. Akizungumza wakati alipotembelea kambi ya timu hiyo, Ofisa Michezo wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Oscar Zabron amesema Serikali imewekeza katika maandalizi ya timu hiyo na sasa inatarajia kuona matokeo chanya.
“Watanzania wote wanawaangalia. Ushindi mtakaoupata ni ushindi wa Watanzania wote. Tunatarajia mkatuletee medali, hususan dhahabu. Serikali imewagharamia kambi, lishe na mahitaji mengine muhimu, sasa ni wakati wa kupambana,” alisema Zabron. SOMA: Serikali kuunga mkono mchezo wa judo
Makamu wa Rais wa Chama cha Judo Tanzania (JATA), Andrew Mlugu, alisema timu ipo katika hali nzuri baada ya kufanya maandalizi ya muda mrefu, jambo ambalo halikuwahi kufanyika kwa miaka mingi kutokana na changamoto za kifedha. Amesema wachezaji wana afya njema, morali ya juu na dhamira ya kufanya vizuri, huku akiishukuru Serikali kwa kuwezesha maandalizi yaliyowapa nafasi ya kuongeza kiwango cha ushindani.
Naye Kocha wa timu ya taifa ya judo, Omary Mgoe amesema timu imeendelea na kambi bila kuvunjwa baada ya kushiriki mashindano mbalimbali ya kimataifa, yakiwemo ya Afrika, Finland na Junior Arabia, hali iliyosaidia kuboresha uwezo wa wachezaji. Ameongeza kuwa wachezaji wengi wana uzoefu wa mashindano makubwa ya kimataifa, ikiwemo ya dunia na mchujo wa Olimpiki, huku benchi la ufundi likifanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza katika mashindano yaliyopita ili kuongeza ushindani wa timu.
