KIGOMA: SERIKALI inatarajia kutumia Sh bilioni 1 kuboresha miundombinu ya vituo vya kulea wazee nchini ili kuwawezesha kuishi katika mazingira bora na kuimarisha ustawi wa maisha yao.

Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhandisi MaryPrisca Mahundi ametoa kauli hiyo leo Julai 14 mkoani Kigoma alipofanya ziara kutembelea kituo cha kulelea wazee Kibirizi Manispaa ya Kigoma Ujiji maarufu ‘SILABU’ ambapo alipata nafasi ya kuzungumza na wazee wanaotunzwa kwenye kituo hicho.

Naibu Waziri huyo amesema serikali inajali mchango wa wazee wao kwa taifa kwa muda wote na ndiyo maana serikali inachukua hatua kuhakikisha wazee hao wanatunza na kulindwa sambamba na kupatiwa bima hizo ili kurahisisha upatikanaji wa matibabu yao.

Awali akisoma taarifa kwa Naibu Waziri, Ofisa Ustawi wa Jamii Mfawidhi wa Kituo cha Makazi ya Wazee Kibirizi SILABU Manispaa ya Kigoma Ujiji, Binura Abbas ameishukuru serikali kwa kuendelea kuboresha makazi ya wazee na kuwezesha kupatikana kwa huduma muhimu ikiwemo malazi, chakula, mavazi na matibabu akiwashukuru wadau mbalimbali kwa kuunga mkono serikali kusaidia kituo hicho.

Akizungumza katika ziara hiyo, Mkuu wa Wilaya Kigoma, Dk.Rashid Chuachua amesema serikali kupitia Halmshauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji inasimamia kwa karibu utoaji huduma za kibinadamu kwa kituo hicho kupitia bajeti za serikali sambamba na kukutana na wadau mbalimbali ambao wamekuwa wakisaidia kuongeza nguvu katika kutoa huduma za kibinadamu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *