Chanzo cha picha, NurPhoto via Getty Images
Rais wa Marekani Donald Trump amesema mataifa ya Ghuba ya Uajemi yanapaswa kulipia ulinzi ambao Marekani inayatoa dhidi ya vitisho kutoka Iran.
“Ndani ya mwezi mmoja tangu siku tulipowashambulia, wangekuwa na silaha ya nyuklia kama tusingefanya hivyo. Kama wangekuwa na silaha ya nyuklia, Israel huenda isingekuwapo tena, na pengine hata Mashariki ya Kati isingekuwa salama.”
Akizungumza na waandishi wa habari, Trump amesema Marekani imekuwa ikitumia fedha nyingi kulinda eneo hilo na kwamba ni wakati wa washirika wake kubeba sehemu ya gharama hizo.
“Nataka tulipwe kwa sababu tunalinda sehemu tajiri sana ya dunia. Tunatumia fedha nyingi, hivyo nchi tunazozilinda zinapaswa kutulipa kwa ulinzi huo.”
Trump ametaja Saudi Arabia, Falme za Kiarabu, Qatar, Bahrain na Kuwait kuwa miongoni mwa mataifa yanayonufaika na ulinzi wa Marekani katika eneo la Ghuba.
Trump pia amedai kuwa Iran ilirusha makombora kuelekea mataifa hayo matano, akisema hatua hiyo inaonesha kuwa viongozi wa Tehran ni “hatari” na kwamba Marekani haitakubali hali hiyo iendelee.
Aidha amesema Marekani itafanya “shambulio jingine kubwa” dhidi ya Iran usiku huo, huku akidai kuwa Tehran sasa inataka kufikia makubaliano baada ya miaka mingi ya mazungumzo.
“Tutafanya shambulio jingine kubwa usiku wa leo. Wanataka kufanya makubaliano… Tumekuwa tukifanya mazungumzo kwa miaka 47, lakini hakuna aliyewahi kuwashambulia kijeshi. Sisi tunawashambulia kwa nguvu sana.”
Kauli hiyo imekuja huku mvutano kati ya Marekani na Iran ukiendelea kuongezeka, baada ya mashambulizi ya kijeshi ya pande zote na vitisho vinavyoendelea kuhusu usalama wa usafiri wa majini katika Mlango wa Bahari wa Hormuz.
Trump pia amedai kuwa Iran ilikaribia kupata silaha ya nyuklia kabla ya mashambulizi ya Marekani, akisema Washington itaendelea kuchukua hatua za kijeshi ikiwa itahitajika.
Iran haijajibu mara moja kauli za Trump. Tehran imekuwa ikisisitiza kuwa mpango wake wa nyuklia ni wa matumizi ya amani na imekuwa ikipinga mashambulizi ya Marekani dhidi ya miundombinu yake.
Soma Zaidi: