
Dar es Salaam. Katika ulimwengu wa sasa unaobadilika kwa kasi, mafanikio ya mwanafunzi hayapimwi tena kwa alama za mitihani pekee.
Ukweli ni kwamba, hata mwanafunzi anayefaulu kwa kiwango cha juu kabisa darasani, anaweza kushindwa kujimudu katika maisha halisi iwapo hatakuwa na stadi kama mawasiliano, nidhamu binafsi, uwezo wa kufanya kazi na wengine, ubunifu, pamoja na uwezo wa kutatua changamoto. Hizi ndizo zinazoitwa stadi za ujuzi laini, kwa kimombo soft skills.
Haya ndiyo maarifa yanayomsaidia mtu kuishi, kufanya kazi na kushirikiana na jamii kwa ufanisi. Na hizi ndizo stadi zinazozungumzwa kwenye ujuzi laini.
Katika soko la ajira la leo, waajiri hawatafuti vyeti pekee; wanatafuta watu wanaoweza kuwasiliana vizuri, wanaoweza kufanya kazi katika timu, wanaoweza kubadilika kulingana na mazingira na wanaoweza kufikiri kwa kina. Hii ina maana kuwa mfumo wa elimu unapaswa kubadilika na kuanza kuandaa wanafunzi kwa uhalisia wa maisha, si kwa mitihani pekee.
Kwa nini ujuzi huu muhimu?
Ujuzi laini ni mkusanyiko wa stadi za kijamii na kihisia zinazomwezesha mtu kuingiliana vizuri na wengine na kufanya kazi kwa ufanisi.
Mfano wa stadi hizi ni pamoja na mawasiliano bora, uongozi, usimamizi wa muda, uvumilivu, ubunifu, pamoja na uwezo wa kudhibiti hisia.
Tofauti na masomo ya darasani ambayo mara nyingi hupimwa kwa mitihani, ujuzi laini huonekana kupitia vitendo na mienendo ya mtu katika maisha ya kila siku. Mwanafunzi mwenye ujuzi huu anaweza kueleza mawazo yake kwa ufasaha, kusikiliza wengine, kushirikiana katika kazi za kikundi na hata kukabiliana na changamoto bila kukata tamaa.
Katika maisha ya kawaida, ujuzi laini humsaidia mtu kujenga uhusiano bora, kufanya uamuzi sahihi na hata kuhimili misukosuko ya maisha.
Kwa mfano, mtu mwenye uwezo wa kudhibiti hisia anaweza kuepuka migogoro isiyo ya lazima, wakati mwenye ujuzi wa mawasiliano anaweza kujenga mtandao mpana wa watu unaoweza kumsaidia katika nyanja mbalimbali.
Kwa upande wa ajira, kazi za kitafiti mbalimbali zimeonyesha kuwa waajiri wengi huweka uzito mkubwa kwa waombaji wenye ujuzi laini kuliko hata wale wenye ufaulu mkubwa, lakini wasio na uwezo wa kushirikiana na wengine au kuwasiliana kwa ufanisi. Hii inaonyesha wazi kuwa elimu bila ujuzi laini ni kama chombo kisicho na mwongozo.
Changamoto tuliyonayo
Licha ya umuhimu wa ujuzi laini, bado shule nyingi zimeendelea kuzingatia zaidi ufaulu wa kitaaluma. Mfumo wa ufundishaji na tathmini umejikita katika mitihani ya kuandika, ambayo hupima zaidi kumbukumbu ya mwanafunzi kuliko uwezo wake wa kufikiri, kuwasiliana au kushirikiana na wengine.
Walimu wengi pia hawapati mafunzo ya kutosha kuhusu namna ya kufundisha ujuzi laini. Hali hii husababisha wanafunzi kumaliza shule wakiwa na vyeti vizuri lakini wakikosa stadi muhimu za maisha.
Ndiyo maana mara nyingi tunaona wahitimu wakishindwa kujieleza vizuri wanapofika kwenye usaili wa kazi, au wakishindwa kuhimili mazingira ya kazi yanayohitaji ushirikiano na ubunifu.
Twende na mwelekeo huu
Ili kubadilisha hali hii, ni muhimu kwa shule kuanza kufundisha ujuzi laini tangu ngazi za awali kabisa za elimu. Watoto wakianza kujifunza tabia na mienendo mapema, ni rahisi kuwajengea misingi imara ya ujuzi huu wakiwa wadogo.
Kwanza, mitalaa inapaswa kujumuisha masomo au vipengele vinavyolenga kukuza ujuzi laini. Hii inaweza kufanyika kwa kuingiza shughuli za vikundi, mijadala darasani, na kazi za ubunifu zinazowahamasisha wanafunzi kufikiri na kushirikiana.
Natarajia haya yamefanyiwa kazi katika maboresho ya mtalaa mpya na mapitio ya Sera ya Elimu ya mwaka 2014.
Pili, walimu wanapaswa kupewa mafunzo maalum ili waweze kufundisha na kutathmini ujuzi laini. Mwalimu anapokuwa na uelewa mzuri wa stadi hizi, ataweza kuzitambua kwa wanafunzi na kuwasaidia kuzikuza kwa njia sahihi.
Tatu, mazingira ya shule yanapaswa kuhamasisha maadili na tabia njema. Shule iwe mahali ambapo wanafunzi wanajifunza kuheshimiana, kushirikiana na kuwajibika. Nidhamu isisitizwe si kwa adhabu kali pekee, bali kwa kuelekeza na kujenga uelewa.
Nne, wazazi nao washirikishwe katika mchakato huu. Malezi ya nyumbani yana mchango mkubwa katika kukuza ujuzi laini. Wazazi wanapaswa kuwafundisha watoto wao maadili, uwajibikaji na namna ya kuwasiliana vizuri na wengine.
Faida kwa jamii
Kama Taifa litawekeza katika kufundisha ujuzi laini, faida zake zitakuwa kubwa na za muda mrefu. Kwanza, tutakuwa na nguvu kazi yenye uwezo wa kufanya kazi kwa ufanisi na kushirikiana vizuri. Hii itaongeza tija katika sekta mbalimbali za uchumi.
Pili, jamii itakuwa na watu wenye maadili na uwezo wa kutatua migogoro kwa njia ya mazungumzo badala ya vurugu. Hii itachangia amani na utulivu katika jamii.
Tatu, vijana watakuwa wabunifu zaidi na wenye uwezo wa kujiajiri. Badala ya kusubiri ajira, wataweza kutumia ujuzi wao kuanzisha miradi na biashara mbalimbali.
Nne, kutakuwa na ongezeko la viongozi bora wanaoweza kusimamia rasilimali na kuongoza kwa uadilifu. Ujuzi laini kama uongozi na mawasiliano ni muhimu sana katika nafasi za uongozi.
Kwa ujumla, elimu ya darasani pekee haitoshi kumwandaa mwanafunzi kwa maisha ya sasa. Ulimwengu unahitaji zaidi ya vyeti; unahitaji watu wenye uwezo wa kufikiri, kushirikiana na kuishi kwa maadili.