
Dar es Salaam. Tanzania haijamnyonga mfungwa yeyote tangu mwaka 1994, lakini mamia ya watu wanaendelea kuishi gerezani wakiwa na hukumu ya kunyongwa.
Mwenendo huo umeendelea kuibua mjadala kuhusu haja, uhalali na umuhimu wa kuwepo kwa adhabu ya kifo ndani ya mfumo wa sheria nchini.
Mjadala huo umeibuliwa upya baada ya kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyoitoa jana, Jumatatu, Julai 13, 2026, aliposema tangu alipoingia madarakani hajawahi kutia saini ya kuruhusu utekelezaji wa adhabu ya kifo.
“Kalamu yangu mimi, hatari yake ni kusaini mtu kunyongwa, na sijawahi kufanya. Baada ya ninyi (mawakili) kupeleleza, kupeleka kesi na kuisimamia, hakimu akaamua akihukumiwa kunyongwa, Rais asaini anyongwe. Sijawahi kufanya,” amesema.
Kauli hiyo si ya kwanza kutoka kwa mkuu wa nchi, kwani Desemba 9, 2020, wakati wa maadhimisho ya Uhuru wa Tanganyika, Rais wa Awamu ya Tano, hayati John Magufuli, alisema hakuwahi kusaini utekelezaji wa adhabu ya kifo licha ya kuwa na mamlaka hayo.
Alisema katika kipindi chake cha uongozi, alipaswa kusaini hukumu za watu 256 waliohukumiwa kunyongwa, lakini hakufanya hivyo na badala yake aliwabadilishia adhabu hiyo kuwa vifungo vya maisha.
“Kwa sababu wapo waliohukumiwa kunyongwa kwa sababu waliuwa. Mwingine aliua mmoja, mwingine aliuwa wawili, mwingine aliuwa watatu. Mimi sheria inaniambia niue 256. Nani mwenye dhambi zaidi? Huyo aliyeuwa wawili au mimi nitakayeuwa 256?” alihoji Magufuli.
Ilitekelezwa kitambo
Adhabu ya kifo ilitekelezwa mara ya mwisho mwaka 1994 chini ya uongozi wa Rais hayati Ali Hassan Mwinyi. Marais wote waliomfuata hawajawahi kuidhinisha utekelezaji wake.
Tangu uhuru wa Tanganyika mwaka 1961, watu 82 pekee ndio walionyongwa kutokana na adhabu hiyo. Kati yao, 10 walinyongwa wakati wa utawala wa Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere.
Awamu ya Pili chini ya hayati Ali Hassan Mwinyi ndiyo iliyoongoza kwa kuidhinisha utekelezaji wa adhabu hiyo. Watu 72 walinyongwa, kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa bungeni mwaka 2008 na aliyekuwa Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe.
Sheria zinaitambua
Licha ya kutotekelezwa kwa zaidi ya miongo mitatu, adhabu ya kifo bado ipo katika sheria za Tanzania. Kifungu cha 197 cha Kanuni za Adhabu kinaeleza kuwa mtu anayepatikana na hatia ya kosa la mauaji atahukumiwa kunyongwa, na adhabu hiyo haina mbadala.
Pia, Kifungu cha 325(3) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, Sura ya 20, kinampa Rais mamlaka ya kuidhinisha utekelezaji wa adhabu hiyo.
Kifungu hicho kinaeleza kuwa:”Rais atatoa hati ya utekelezaji wa adhabu ya kifo (death warrant), au amri ya kubadilisha adhabu hiyo, au msamaha, kwa sahihi yake na muhuri wa Jamhuri ya Muungano ili kutekeleza uamuzi huo.”
Mei 2023, gerezani kulikuwa na wafungwa 691 waliohukumiwa adhabu ya kifo, kwa mujibu wa Ripoti ya Tume ya Haki Jinai iliyoongozwa na Jaji Othman Chande.
Imeshapingwa mara kadhaa
Wakati marais wa karibuni wakionekana kutoidhinisha utekelezaji wa adhabu hiyo, sauti za kutaka sheria ibadilishwe zimeendelea kujitokeza ndani na nje ya nchi.
Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (AfCHPR) iliiagiza Tanzania kufanya marekebisho ya Kanuni za Adhabu ndani ya mwaka mmoja ili kuondoa sharti la lazima la adhabu ya kunyongwa kwa anayepatikana na hatia ya mauaji.
Mahakama hiyo ilisema adhabu ya lazima ya kunyongwa inakiuka haki ya kuishi inayolindwa na Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu, ambao Tanzania imeuridhia.
Uamuzi huo ulitokana na kesi namba 007 ya mwaka 2015 iliyofunguliwa na Ali Rajab, Angaja Kazeni, Geofrey Stanley, Emmanuel Michael na Julius Petro, waliohukumiwa adhabu ya kifo na Mahakama Kuu mwaka 2011 kwa kosa la mauaji.
Mbali na uamuzi huo wa mahakama, Tume ya Haki Jinai, mwaka 2023, pia ilipendekeza mabadiliko ya mfumo wa adhabu ya kifo, ilishauri adhabu hiyo isiwe ya lazima kwa wote wanaopatikana na hatia ya mauaji.
Aidha, ilipendekeza kwamba endapo adhabu ya kifo haitaidhinishwa na Rais ndani ya miaka mitatu tangu hukumu itolewe, ibadilishwe moja kwa moja kuwa kifungo cha maisha.
Ni adhabu mbaya, katili
Akizungumza na Mwananchi leo, Jumanne, Julai 14, 2026, Mtaalamu wa Sheria, Dk Said Mandia, amesema kinachoonekana kuhusu adhabu hiyo ni kwamba ni mbaya, kwa sababu hata wanaotakiwa kuitekeleza wanasita kufanya hivyo.
“Hii adhabu inawezekana si nzuri kwa sababu hata wanaotakiwa kuitekeleza wanaiogopa,” amesema Dk Mandia.
Anasema Tume ya Haki Jinai iliyoundwa na Rais Samia iliwahi kupendekeza kuwa iwapo adhabu hiyo haitatekelezwa kwa miaka mitatu, ibadilishwe kuwa kifungo cha maisha gerezani.
Dk Mandia amesema adhabu hiyo inaonekana kuwa ya kikatili, kwa kuwa inaweza kumdhalilisha hata mtekelezaji.
“Kwa mfano, wewe ni askari umepewa kazi ya kunyonga. Unaweza ukarudi nyumbani ukamsimulia mkeo leo nimefanya kazi sana?” amehoji.
Amesema adhabu hiyo ni mbaya kwa kuwa hakuna anayejisikia fahari kuitekeleza, na kwamba kumekuwa na juhudi za kutaka ifutwe.
Licha ya shinikizo la kutaka adhabu hiyo ifutwe, Dk Mandia amesema inaonekana wananchi wengi wanatamani iendelee kuwapo, akirejea maoni yaliyotokana na tume mbalimbali, ikiwamo ya Jaji Nyalali, ya Jaji Warioba na ile ya kurekebisha sheria.
“Imeonekana kama wananchi hawataki adhabu ifutwe, lakini wanaharakati na baadhi ya wadau wa sheria wanapendekeza ifutwe,” amesema.
Wanaotaka ifutwe, amesema, wanajenga hoja ya ukiukaji wa haki ya kuishi, huku wasiotaka ifutwe wakihofia ongezeko la matukio ya mauaji.
Amekwenda mbali zaidi na kusema kuwa kuna baadhi ya nchi zilifuta adhabu hiyo, lakini baadaye zikajikuta makossa hayo ya mauaji yakiongezeka.
Imepitwa na wakati
Mhadhiri Mwandamizi wa Sheria wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Leodard Shaidi, amesema adhabu hiyo imepitwa na wakati.
Amesema kuna nchi chache duniani zinazoendelea kuitekeleza, sambamba na baadhi ya majimbo ya Marekani, lakini sehemu nyingine nyingi duniani imefutwa.
Kwa upande wa Tanzania, amesema mamlaka zinakwama kuifuta kwa sababu zinaona kuwa, kwa mtazamo uliopo, ikitangazwa imefutwa huenda matukio ya mauaji yakaongezeka.
“Sasa leo ukisema adhabu ya kifo imefutwa, maana yake ukiuwa hutauawa. Pengine inaonekana watu wakiwa na mtazamo huo, mauaji yataongezeka,” amesema.
Hata hivyo, amesema kwa maoni yake, adhabu hiyo imepitwa na wakati na inapaswa kufutwa.
Iendelee kupunguza ukatili
Kwa upande wake, mkufunzi wa masuala ya malezi, Maria Deus, amesema kutokana na tabia na mfumo wa maisha ya Watanzania, ni muhimu sheria hiyo iendelee kuwapo ili kabla mtu hajamuua mwenzake, atambue kuwa naye anaweza kuhukumiwa adhabu hiyo.
“Isipokuwepo, suala la kuuwa litakuwa holela. Mtu atajua nitauwa, ataishi. Kwa hali hii ya maisha na matukio tunayoendelea kuyasikia, ikifutwa hali itakuwa mbaya,” amesema.
Hata ikitokea Serikali ikataka kuifuta, Maria amesema ianze kwa kufanya tathmini ya hali ya jamii, ikiwamo mtazamo wa wananchi na madhara yanayoweza kujitokeza endapo adhabu hiyo itaondolewa.