GEITA: CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Geita kimewataka watumishi katika sekta ya afya kuzingatia weledi katika matumizi sahihi ya dawa na vifaa tiba ili wananchi wote wapate uhakika wa huduma za afya.

Kaimu Katibu wa CCM wa Mkoa, Walid Josephat amesema hayo kwa niaba ya chama alipoongoza Kamati ya Siasa ya Mkoa kukagua Ujenzi wa Bohari ya Dawa (MSD) Hospitali ya Kanda Chato.

Walid amesema dhamira ya serikali kuwekeza sh bilioni 19 kujenga kituo cha MSD Chato ni kuongeza uhakika wa upatikanaji wa dawa na vifaa tiba na kuboresha huduma za afya nchini.

“Kikubwa wale ambao watakuwa wanahudumia hapa waache ubadhirifu, wawe waaminifu na kuhakikisha dawa zinapatikana wakati wote.

“Haitakuwa na maana kuwa na bohari ya dawa kubwa na ya kisasa, harafu tukose dawa huko mitaani kwenye vituo vyetu vya afya pamoja na zahanati”, amesema Walid.

Amesema serikali ya CCM inatambua ongezeko la idadi ya watu mkoani Geita na hivo ujenzi wa MSD Chato unatarajia kukidhi mahitaji ya huduma za dawa na vifaa tiba.

Walid amesema halmashauri zinapaswa kuwajibika kikamirifu kudhibiti urasimu wa dawa na vifaa tiba na pia kuharakisha mchakato wa usambazaji wa dawa ili kuepuka uhaba wa dawa vituoni.

Mkuu wa mkoa wa Geita, Martine Shigela amesema ujenzi wa kituo cha MSD Chato ni sehemu ya miradi ya kimkakati inayolenga kutatua changamoto za kijamii na kuboresha huduma za afya.

Shigela amesema serikali inafuatilia kwa ukaribu maendeleo ya mradi huo ulioanza Agosti 20, 2025 ili kuhakikisha unakamilika kwa wakati kwa mjibu wa mkataba.

Meneja wa MSD Kanda ya Chato, Masatu Kalendelo amesema mradi wa MSD Chato unahusisha ujenzi wa ghala lenye Mita za Mraba 4,800, litakalohudumia mikoa ya Geita, Kagera na Kigoma.

Masatu amesema Wizara ya Afya imeweka utaratibu mzuri kudhibiti uchepushaji wa dawa ambapo zahanati na vituo vya afya vitapaswa kuomba dawa kupitia halmashauri kwenda MSD.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *