Kigoma. Walimu, wanafunzi na wananchi wa Mkoa wa Kigoma wanatarajiwa kunufaika na mapinduzi ya matumizi ya teknolojia katika elimu baada ya Shirika la Enabel kutoka Ubelgiji kukabidhi madarasa matatu ya kisasa yanayohamishika (Digitruck) yenye thamani ya Sh600 milioni.
Madarasa hayo yameunganishwa na mfumo wa intaneti na yamewekewa nishati ya sola pamoja na kompyuta mpakato, hatua inayotarajiwa kurahisisha ufundishaji na ujifunzaji wa kidijitali hata katika maeneo yenye changamoto ya upatikanaji wa umeme.
Kupitia miundombinu hiyo, walimu watapata mafunzo ya matumizi ya teknolojia darasani, huku wanafunzi wakiongeza uwezo wa kujifunza kwa kutumia Tehama na kupata maarifa yanayokidhi mahitaji ya dunia ya sasa.
Mbali na sekta ya elimu, vituo hivyo vinatarajiwa kuwa chachu ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa kuwapatia vijana ujuzi wa kidijitali, kuwasaidia wajasiriamali kujifunza biashara za mtandaoni, wakulima kupata maarifa ya kilimo cha kisasa kupitia teknolojia na wananchi kupata mafunzo mbalimbali yanayochochea maendeleo.
Mkurugenzi wa Shirika la Enabel nchini Tanzania, Geokint Koenraad, akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi madarasa ya kisasa yanayohamishika.
Madarasa hayo yamekabidhiwa kwa wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya za Kasulu, Kibondo na Kigoma, ambapo yatawekwa katika vituo vya rasilimali za walimu vya Nyansha TC wilayani Kasulu, Kizazi wilayani Kibondo na Bitale wilayani Kigoma ili kurahisisha upatikanaji wa mafunzo ya kidijitali kwa walimu.
Makabidhiano hayo yalifanyika Julai 14, 2026 katika Kata ya Nyansha, Wilaya ya Kasulu, yakihudhuriwa na viongozi wa Mkoa wa Kigoma pamoja na wawakilishi wa Enabel kutoka Tanzania, Kenya, Uganda na Rwanda.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Balozi mstaafu Simon Sirro, Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Kanali Isaac Mwakisu, alisema uwekezaji huo utaongeza ubora wa elimu na kuwataka walimu pamoja na viongozi wa halmashauri kuhakikisha vifaa hivyo vinatunzwa ili viendelee kuwahudumia walengwa kwa muda mrefu.
“Vifaa hivi vitawasaidia walimu kutumia teknolojia katika kufundisha, wanafunzi kupata elimu inayokwenda sambamba na dunia ya kidijitali, vijana kuongeza ujuzi wa Tehama, wajasiriamali kujifunza biashara za kidijitali na wakulima kupata maarifa ya kilimo cha kisasa kupitia teknolojia.
Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Kanali Isaac Mwakisu, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, IGP Mstaafu Balozi, Simon Sirro, akizungumza wakati wa hafla ya kupokea madarasa ya kisasa yanayohamishika, yaliyotolewa na Shirika la Enabel ya nchini Ubelgiji.
“Hata wananchi kwa ujumla watanufaika kupitia mafunzo mbalimbali yatakayochochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi,” alisema Kanali Mwakisu.
Mtaalamu wa masuala ya kidijitali wa Enabel, Walter John, alisema kila darasa lina kompyuta mpakato 21 pamoja na mfumo wa nishati ya sola ili kuhakikisha huduma zinaendelea hata kunapotokea changamoto za umeme.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Enabel nchini Tanzania, Geokint Koenraad, alisema vituo hivyo vitawajengea walimu uwezo wa kutumia teknolojia katika ufundishaji na kuongeza ubora wa elimu kupitia ushirikiano wa kikanda.
Uwekezaji huo unakuja wakati Serikali ikiendelea kuhimiza matumizi ya teknolojia katika sekta ya elimu kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kujenga mfumo wa elimu unaotumia teknolojia kuongeza ubora wa ufundishaji, ujifunzaji na upatikanaji wa maarifa kwa Watanzania.