Babati. Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Regina Ndege amekabidhi mifuko 100 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa uzio wa Hospitali ya Dareda Mission ya Wilaya ya Babati mkoani Manyara.
Hatua hiyo imekuja baada ya kuwapo kwa changamoto ya hospitali hiyo kongwe kutokuwa na uzio hali iliyokuwa ikihatarisha usalama wa wagonjwa na mali, ambapo kufuatia hilo, Ndege aliahidi kuujenga ili kuboresha mazingira ya utoaji wa huduma.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumatano Julai 15, 2026 Ndege amesema huo ni utekelezaji wa ahadi aliyoitoa kwa uongozi na watumishi wa hospitali kwenye maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani (Mei Mosi) mwaka huu, baada ya kubaini ukosefu wa uzio ulikuwa miongoni mwa changamoto kubwa zinazoikabili hospitali hiyo.
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Regina Ndege (kushoto) akikabidhi mifuko 100 ya saruji kwa mkurugenzi wa hospitali ya Dareda Mission ya wilayani Babati mkoani Manyara, Padri Peter Salaho. Picha na Joseph Lyimo
“Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuboresha huduma za afya nchini ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora katika mazingira salama na rafiki,” amesema Ndege.
Amesisitiza wadau pamoja na wananchi kuendelea kusimamia ipasavyo miradi yote inayotekelezwa na Serikali ili ijengwe kwa viwango vinavyotakiwa na iakisi thamani ya fedha iliyotolewa.
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Regina Ndege (kushoto) akipongezwa baada ya kukabidhi mifuko 100 ya saruji na Diwani wa kata ya Dareda, Wilbroad Bayo. Picha na Joseph Lyimo
Mkurugenzi wa hospitali hiyo, Padri Peter Saraho, ameishukuru Serikali kwa mchango huo mkubwa, akisema utasaidia kuimarisha usalama na kuboresha mazingira ya utoaji wa huduma.
Diwani wa kata ya Dareda, Willbrod Bayo amempongeza na kumshukuru Naibu Waziri Ndege kwa kutimiza ahadi yake ya kutoa mifuko 100 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa uzio wa hospitali hiyo.