Washington. Maseneta wa Chama cha Democratic nchini Marekani wamekwamisha hatua ya kusonga mbele kwa Muswada wa mwaka wa Sera ya Ulinzi (National Defense Authorization Act–NDAA), wakieleza wasiwasi wao kuhusu kuendelea kwa sera za kijeshi dhidi ya Iran.

Muswada huo ulipata uungwaji mkono wa maseneta 50 huku 46 wakiupinga, matokeo yaliyoshindwa kufikia kiwango kinachohitajika kuendelea na hatua zinazofuata za mchakato wa kutungwa sheria.

Hatua hiyo imeonyesha mgawanyiko mkubwa ndani ya Seneti kuhusu mwelekeo wa sera ya Marekani kwa Iran na namna bajeti ya Wizara ya Ulinzi inavyoweza kutumika kufadhili operesheni za kijeshi.

Seneta, Richard Blumenthal ambaye ni  mwanachama wa Chama cha Democratic na kiongozi wa upinzani katika Kamati ya Seneti ya Huduma za Kijeshi, amesema muswada huo unaendeleza ufadhili wa vita dhidi ya Iran bila kuwepo kwa uwajibikaji wa kutosha kutoka kwa utawala wa Rais Donald Trump.

“Kwa mtazamo wangu, sheria hii inaendeleza ufadhili wa vita, huku utawala wa sasa ukikosa uwajibikaji,” amesema Blumenthal.

Amesema hataunga mkono muswada huo hadi utawala wa Trump utoe mkakati wa wazi kuhusu Iran na upate idhini ya Bunge kwa mujibu wa Sheria ya Mamlaka ya Vita.

Kwa upande wake, Seneta Tammy Duckworth amesema hataupigia kura muswada huo isipokuwa marekebisho aliyowasilisha yapitishwe. Marekebisho hayo yanalenga kuzuia fedha zaidi za serikali kutumika kufadhili operesheni za kijeshi zinazolenga Iran.

Muswada wa NDAA ni miongoni mwa sheria muhimu zinazobainisha sera na matumizi ya bajeti ya ulinzi ya Marekani kwa mwaka wa fedha, hivyo hatua ya kukwamishwa kwake inaashiria mvutano unaoendelea kuhusu sera za usalama na matumizi ya nguvu za kijeshi nje ya nchi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *