Hai. Sauti ya mapokezi na matarajio mapya ya utalii imetawala leo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), baada ya ndege ya Shirika la Ndege la Neos kutoka Italia kutua kwa mara ya kwanza, ikiwa imebeba zaidi ya watalii 210 waliokuja kutembelea vivutio mbalimbali nchini.
Kutua kwa ndege hiyo leo Jumatano, Julai 15, 2026, kumeashiria mwanzo wa safari za moja kwa moja kati ya Italia na Kilimanjaro, hatua inayotarajiwa kuongeza idadi ya wageni kutoka soko la Ulaya na kuchochea shughuli za utalii na biashara katika Kanda ya Kaskazini.
Miongoni mwa waliokuwa uwanjani kuipokea ndege hiyo ni Meneja wa Masoko na Utafiti wa KIA, Zefrin Lubuva ambaye amesema ujio wa ndege hiyo ni hatua muhimu katika kukuza sekta ya utalii na uchumi wa eneo la Kaskazini ya Tanzania.
“Tumepokea ndege ya Neos kutoka Italia ambayo itafanya safari za moja kwa moja hadi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro. Hili ni tukio kubwa linaloongeza idadi ya mashirika ya ndege ya kimataifa kutoka Ulaya yanayofika Kilimanjaro,” amesema Lubuva.
Baadhi ya watalii waliowasili nchini kwa ndege ya Shirika la Ndege la Kimataifa la Neos kutoka Italia wakishuka katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) baada ya ndege hiyo kutua kwa mara ya kwanza katika uwanja huo leo, Julai 15, 2026.
Amesema huduma hiyo mpya ina umuhimu mkubwa kiuchumi kutokana na uwezo wa ndege hiyo kubeba idadi kubwa ya watalii kwa safari moja, jambo litakaloongeza fursa kwa sekta mbalimbali zinazotegemea utalii.
“Ndege hii leo imeshusha zaidi ya wageni 210 ambao wanaelekea katika vivutio mbalimbali. Hii ni fursa kubwa kwa sekta ya utalii, biashara katika Kanda ya Kaskazini na Taifa kwa ujumla.”
“Tunaamini msimu huu mkubwa wa utalii utawanufaisha wananchi wengi kupitia biashara na ajira zitakazotokana na ongezeko la wageni,” amesema Lubuva.
Mkurugenzi wa KIA, Rehema Myeya amesema ujio wa huduma hiyo utarahisisha safari za watalii wanaokuja nchini na kuongeza fursa za kiuchumi kwa wananchi na wafanyabiashara.
“Huduma hii mpya ya ndege itasaidia wageni kufika kwa urahisi kwenye vivutio vyetu vya utalii kupitia KIA. Pia itaongeza fursa za biashara kwa wazawa na wafanyabiashara wakubwa,” amesema.
Naye mwakilishi wa Shirika la Ndege la Neos nchini Tanzania, Antonella Balestra amesema kampuni hiyo inafurahia kuanza safari za moja kwa moja hadi Kilimanjaro, akieleza kuwa tayari imekuwa ikitoa huduma Zanzibar tangu mwaka 2022.
“Tunafurahi sana kuwa leo ni mara yetu ya kwanza kutua Kilimanjaro. Tayari tumekuwa tukifanya safari za Zanzibar tangu mwaka 2022 na tunatarajia kuongeza idadi ya safari kulingana na mahitaji ya abiria wetu, hasa katika kipindi hiki cha msimu mkubwa wa utalii,” amesema Balestra.
Kwa baadhi ya watalii waliofika na ndege hiyo, wamesema safari yao ilianza kwa matarajio makubwa ya kujionea uzuri wa Tanzania.
Eliza Saminar, mmoja wa watalii hao amesema, “tumekuja kutembelea maeneo mbalimbali. Tanzania ni nchi nzuri yenye mandhari ya kuvutia, na tunafurahia kuwa hapa.
Ujio wa Neos unaongeza idadi ya mashirika ya ndege ya kimataifa yanayounganisha Tanzania na masoko ya nje, huku wadau wa utalii wakitarajia hatua hiyo kuongeza wageni, mapato na fursa za ajira katika msimu huu wa utalii.