
Iran imeonya kwamba italenga kila miundombinu iliyosalia katika eneo hili iwapo miundombinu yake itashambuliwa.
Katika taarifa kali, Makao Makuu ya Kamandi ya Majeshi ya Iran maarufu kama Kamandi ya Khatam al-Anbiya, imeonya kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wavamizi. Indhari hiyo imetolewa siku ya Alhamisi, baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kutishia kupanua mashambulizi ya kigaidi ya Marekani dhidi ya Iran wiki ijayo ili yalenge miundombinu ya kiraia, ikiwemo vituo vya umeme na madaraja.
Msemaji wa kamandi hiyo ya kijeshi, Luteni Kanali Ebrahim Zolfaqari, alisema: “Iwapo vitisho vya hivi karibuni visivyo na msingi vya rais wa Marekani vya kuliamuru jeshi la Marekani lilenge miundombinu ya Jamhuri ya Kiislamu vitatekelezwa, basi kila kitu ambacho, kwa sababu ya subira na kujizuia kwa Iran, kimebakia salama hadi sasa, yaani miundombinu yote katika eneo hili, kitapondwa chini ya mapigo ya chuma ya vikosi vya kijeshi vyenye nguvu vya Jamhuri ya Kiislamu, kwa kiwango ambacho hakutabaki athari yoyote yake, kana kwamba hakikuwahi kuwepo.”
Aidha, ameukosia utawala wa kihalifu wa Marekani kwa kuendelea na vitendo vyake vya kiholela na juhudi zake za kuleta machafuko katika Asia Magharibi.
Kanali Zolfaqari alisisitiza zaidi kwamba Iran haitairuhusu kamwe , kama nchi ya kigeni iliyo nje ya eneo hili, kuingilia Lango la Hormuz, ambalo ni “mstari mwekundu usiokiukwa” wa Jamhuri ya Kiislamu.
Ameongeza kwamba: “Adui mjinga na ajue: kwetu sisi, wakati wa hatua za kishujaa si wakati wa kujizuia. Kinachotekelezwa na vikosi vya ulinzi vya Iran si shambulio la kulipiza kwa kiwango sawa; ni shambulio lenye ubora na nguvu ya juu zaidi. Mashambulizi yatakuwa makali zaidi, mapana zaidi, na yenye uharibifu mkubwa kuliko wakati wowote uliopita. Ghadhabu ya taifa ambalo halijawahi kusalimu amri itamteketeza mvamizi.”
Kwingineko siku ya Alhamisi, Idara ya Uhusiano wa Umma ya Jeshi la Iran la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) imetangaza kwamba Jeshi la Wanamaji la kikosi hicho limefanya “shambulio lenye kuangamiza dhidi ya kambi ya kijeshi ya Marekani ya Sheikh Isa nchini Bahrain.”
IRGC imesema kwamba operesheni hiyo imeharibu kikamilifu mfumo wa rada wa ufuatiliaji na udhibiti wa anga pamoja na kituo cha kusukuma mafuta kilichokuwa kikiyapatia ndege za kivita za adui huduma ya mafuta.
Shambulio hilo lilikuja kujibu jinai za jeshi la Marekani linaloua watoto, katika mashambulizi yake ya angani dhidi ya kambi za pwani na maeneo kadhaa ya kiraia, ikiwemo hospitali ya saratani ya watoto na kituo cha uzalishaji maji kilichokuwa kikihudumia mazuwari wanaosafiri kuelekea mji mtakatifu wa Karbala nchini Iraq katika eneo la mpakani la Mkoa wa Ilam wa Iran.
Katika siku chache zilizopita, mvutano umeongezeka katika Mlango wa Hormuz, kutokana na mashambulizi ya kigaidi ya Marekani dhidi ya Iran, katika ukiukaji mkubwa wa makubaliano ya kumaliza vita ya mwezi uliopita kati ya pande hizo mbili.
Iran imetangaza njia hiyo ya kimkakati ya majini kuwa imefungwa “hadi itakapotolewa taarifa nyingine” na angalau hadi “mwisho wa uingiliaji wa Marekani katika eneo hili.”