Morogoro. Wananchi wa Kijiji cha Mtimbira, Wilaya ya Malinyi mkoani Morogoro, wameusimamisha msafara wa Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, wakimlalamikia kuhusu ubovu wa barabara ya Ifakara–Lupilo–Mtimbira–Malinyi uliodumu kwa zaidi ya miaka kumi.
Wanakijiji hao walilazimika kuusimamisha msafara huo kwa takriban dakika 20 jana Julai 15,2026 wakitaka awasikilize kilio chao cha muda mrefu wakitaka barabara hiyo ijengwe kwa kiwango cha lami.
Hatua hiyo imekuja baada ya wananchi wa eneo hilo kukumbwa na changamoto za mawasiliano kutokana na ubovu wa barabara, kusombwa kwa madaraja kila msimu wa mvua, hali inayosababisha kuchelewesha usafirishaji wa mazao na kuathiri upatikanaji wa huduma muhimu za kijamii.
Wananchi hao walijipanga kandokando ya barabara wakiwa na mabango baadhi yakisomeka, “Serikali yetu tunaipenda sana, kilio chetu ni lami; tukipata lami tumepata maendeleo,” huku wakicheza ngoma za asili na kuuzuia msafara huo kupita hadi Waziri Ulega aliposhuka na kuzungumza nao.
Wananchi hao walisema waliamua kuzuia msafara huo kwa hofu kuwa usingesimama wakati wa kurejea, hivyo waliona ni fursa ya pekee kufikisha kilio chao moja kwa moja kwa Waziri.
Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega akizungumza jambo na wananchi wa kijiji cha Mtimbira baada ya wananchi hao kuzuia msafara wake wakati akiwa katika ziara ya kukagua miundombinu ya barabara Wilaya ya Malinyi mkoani Morogoro. Picha na Juma Mtanda
Walisema ubovu wa barabara hiyo kwa miaka mingi umekuwa ukiongeza gharama za usafiri, kuchelewesha usafirishaji wa mazao na kuathiri huduma za afya, elimu na biashara.
Akiongezea uzito kauli ya wananchi, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima, alisema changamoto ya miundombinu ya barabara ni miongoni mwa vikwazo vikubwa vinavyoikabili Wilaya ya Malinyi katika kufikia maendeleo.
Malima alisema wakati wa mvua, safari kutoka Ifakara hadi Malinyi huongezeka kwa muda mrefu kutokana na ubovu wa barabara na uharibifu wa madaraja.
Alisema Serikali imeendelea kuhakikisha barabara hiyo inapitika katika misimu yote huku ikiendelea na maandalizi ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi kwa kiwango cha lami.
“Barabara hii ni muhimu kwa uchumi wa Wilaya ya Malinyi na Mkoa wa Morogoro kwa ujumla. Itarahisisha usafirishaji wa mazao, kuongeza biashara na kuwaunganisha wananchi na huduma muhimu za kijamii,” alisema Malima.
Wananchi wakifuatilia jambo wakati Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega (hayupo pichani) katika kijiji cha Mtimbira wakati wa ziara ya waziri huyo aliyekuwa akikagua miundombinu ya barabara ya Lupili wilaya ya Ulanga na wilaya ya Malinyi mkoani Morogoro. Picha na Juma Mtanda
Akizungumza na wananchi hao, Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, alisema Serikali tayari imepata mkandarasi mpya wa kutekeleza mradi huo baada ya mkandarasi wa awali kushindwa kuendelea na kazi.
Alisema fedha za kuanza utekelezaji wa mradi zimetengwa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2026/27 na kwamba hatua zinazofuata ni kukamilisha taratibu ili ujenzi uanze.
“Nimewasikiliza na nimeelewa changamoto zenu. Serikali inalitambua tatizo hili na imeanza hatua za utekelezaji wa mradi. Tunataka kuona barabara hii inajengwa ili kuondoa changamoto zinazowakabili wananchi wa Malinyi,” alisema Ulega.
Kwa upande wake, Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Morogoro, Josephine Kapoma, alisema kitendo cha wananchi kuusimamisha msafara wa waziri hakikulenga kuleta taharuki, bali kilikuwa njia ya kuwasilisha kwa utulivu kilio cha muda mrefu kuhusu changamoto ya miundombinu.
Alisema ubovu wa barabara hiyo umeendelea kudhoofisha shughuli za uzalishaji na biashara licha ya Wilaya ya Malinyi kuwa miongoni mwa maeneo makubwa yanayozalisha mazao ya chakula.
“Wananchi wameonyesha kwa utulivu namna wanavyohitaji maendeleo. Kukamilika kwa barabara hii kutarahisisha usafirishaji wa mazao, kuvutia uwekezaji na kuboresha uchumi wa wananchi,” alisema Kapoma.
Mkazi wa Kijiji cha Mtimbira, Hamisi Bakari, alisema wananchi waliamua kuuzuia msafara huo ili wapate nafasi ya kuwasilisha moja kwa moja changamoto yao ya muda mrefu.
Moja ya bango lenye ujumbe tukipata lami tumepata maendeleo kufuatia wananchi kuzuia msafara wa Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega kijiji cha Mtimbira wakati wa ziara ya waziri huyo aliyekuwa akikagua miundombinu ya barabara ya Lupili wilaya ya Ulanga na wilaya ya Malinyi mkoani Morogoro. Picha na Juma Mtanda.
“Tuliamini tukimpata waziri ana kwa ana atasikiliza kilio chetu. Ujumbe tuliouandika kwenye mabango ulikuwa wa kuonyesha kwamba tuna imani na Serikali, lakini tunahitaji kuona utekelezaji wa ujenzi wa barabara. Tukipata lami tutakuwa tumepata maendeleo tunayoyasubiri kwa muda mrefu,” alisema Hamisi.
Barabara ya Ifakara–Lupilo–Mtimbira–Malinyi ni miongoni mwa miradi inayotarajiwa kuboresha mawasiliano katika Wilaya ya Malinyi kwa kurahisisha usafirishaji wa mazao ya kilimo na bidhaa nyingine, kuongeza fursa za biashara na kuboresha upatikanaji wa huduma za afya, elimu na huduma nyingine za kijamii.
Kwa sasa, baadhi ya maeneo ya barabara hiyo hukatika kabisa wakati wa mvua kutokana na kuharibika kwa miundombinu, hali inayowalazimu wananchi kutumia muda mrefu kufikia masoko na huduma muhimu.