Waziri Mkuu wa Malaysia, Anwar Ibrahim, amesema Muisraeli yeyote atakaopatikana akiingia nchini humo atafukuzwa mara moja. Amesema hayo huku mamlaka za Malaysia zikichunguza ripoti kwamba Waisraeli walitumia hati mbili za kusafiria kuingia katika jimbo la kusini la Johor.

“Tunafanya uchunguzi. Haturuhusu hilo. Iwapo lipo, hatua lazima zichukuliwe. Kwa sababu hatutambui (Israel), watafukuzwa mara moja,” alisema Anwar Ibrahim jana Jumatano.

Waziri Mkuu wa Malaysia amesema hayo kufuatia ripoti kwamba Mwisraeli mwenye pasipoti mbili za kusafiria ameingia jimbo la Johor.

Serikali ya jimbo hilo pia imeitaka Wizara ya Mambo ya Ndani na mashirika husika kuchunguza usimamizi wa Shule ya Mtandao huko Forest City, ambayo imedaiwa kuwa na uhusiano na Waisraeli.

Malaysia, ambayo ni mtetezi mkubwa wa harakati za kupigania ukombozi za Palestina, haiitambui Israel na inawazuia watu wenye pasipoti za Israel kuingia nchini humo.

Nchi kadhaa, ikiwa ni pamoja na Indonesia, Pakistan, Algeria, Iraq, Lebanon, Syria, Yemen, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kadhalika, haziitambui Israel na hazina uhusiano wowote wa kidiplomasia na utawala huo haramu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *