Dar es Salaam. Imepita miaka 10 tangu AY alipoachia remix ya wimbo wake, Zigo (2016) akimshirkisha Diamond Platnumz, mshindi mara nane wa tuzo za African Entertainment Awards USA (AEAUSA) zinazofanyika New Jersey, Marekani.
AY, mwanachama wa zamani wa makundi ya S.O.G na East Coast Team, hadi sasa Zigo Remix (2016) unasalia kuwa wimbo wake pekee wenye mafanikio makubwa katika majukwaa ya kidijitali (digital streaming) kwa muda wote.
Huo ni wimbo uliopita katika mikono ya watayarishaji muziki watatu wakubwa katika Bongofleva ambao ni Marco Chali, Nahreel, na Hermy B, mwanzilishi wa Bxtra Records, zamani B’Hits Music Group.
Hata hivyo, AY na Diamond walisafiri hadi Afrika Kusini kwa ajili ya kushuti video ya wimbo huo wakati bado hawajaurekodi!. Baada ya kuwasili huko kwa Madiba, ndipo Hermy B akafunga vifaa katika chumba cha hotel kisha wakarekodi.
Tofauti na maana inayoweza kuhisiwa na wengi, kwa AY ametumia neno lisilo rasmi ‘Zigo’ kuelezea uzuri wa mwanamke ambaye anatamani kupata nafasi ya kuwa naye katika uhusiano.
Video ya wimbo huo iliongozwa na Director Alessio Bettochi chini ya kampuni yake ya Studio Space Pictures (SSP), Alessio alikuwa ni director mwingine wa Afrika Kusini kufanya kazi na AY baada ya Godfather.
Ikumbukwe AY ndiye msanii wa kwanza Bongo kufanya kazi na Godfather, kisha wakafuata wengine kama Alikiba (Mwana), Diamond (Nana), Shetta (Kerewa), Linah (Ole Themba) n.k.
Hatimaye video ya Zigo Remix iliachiwa hapo Januari 22, 2016, na ndani wiki moja ikawa imetazamwa (views) mara milioni 1 YouTube, zikiwa ni namba za juu na za kushtua kwa wakati huo.
Miezi miwili baadaye ikawa imetazamwa mara 5 katika mtandao huo ikiwa ni video ya kwanza ya muziki kufanya hivyo ndani ya Bongofleva, huku ikishika nafasi ya kwanza katika chati za kituo cha Trace TV.
Ikiwa ni miaka 10 imepita tangu rekodi hizo kuandikwa, hakuna wimbo mwingine wa AY uliofanikiwa kufanya hivyo licha ya kutoa kazi nyingi na hata kushirikiana na wasanii mbalimbali wenye ushawishi mkubwa.
Hadi sasa video ya Zigo Remix ikiwa imetazamwa YouTube mara milioni 30.8, video ya pili yake AY inayofuatia kwa kufanya vizuri katika mtandao ni ya wimbo wake, Yule Remix (2024) akimshirikisha Marioo, hii imefikia milioni 1.6.
Kwa muktadha huo, AY ana mzigo mkubwa wa kuja kuzifikia rekodi alizoziweka yeye mwenyewe kupitia wimbo wake, Zigo Remix (2016) hasa rekodi hii ya video, video ambayo mwishoni walionekana Rayvanny na Fid Q.
Hata hivyo, kuna wasanii wengi Bongo ambao nyimbo walizoshirikiana na Diamond zina rekodi ya kufanya vizuri zaidi kiasi kwamba wamekuja kupata ugumu kuzifikia rekodi za aina hiyo.
Baadhi yao ni Chege (Waache Waoane), Linex (Salima), Harmonize (Kwangwaru), Navy Kenzo (Katika), Jux (Enjoy), G Nako (Komando), Barnaba (Salama), na Mr. Flavour (Time To Party) kutokea Nigeria.
Hivyo pia mzigo haupo kwa AY peke yake, wapo wengi ambao ushawishi wa Diamond uliopelekea kolabo zao kuwa kubwa na maarufu, sasa unawapa changamoto ya kutengeneza nyimbo au kolabo nyingine za aina hiyo.
AY, mwanzilishi wa Unity Entertainment, alitoka rasmi kimuziki kupitia wimbo wake, Ni Raha Tu (2001) uliotayarishwa Bongo Records na P-Funk Majani, zamani DJ Skills of Pain.
Kwa mujibu wa AY, nyimbo ambazo amerekodi Bongo Records hakuwahi kuzilipia fedha kutokana na ukaribu wake na P-Funk ambaye aliamua kufanya hivyo kutokana na kusapoti kipaji chake.
Ziara yake ya kwanza kimuziki alipewa nafasi ya Professor Jay, ni katika ziara ya albamu yake, Machozi Jasho na Damu (2001), hapa ndipo AY alipozunguka sana nchi akiwa msanii wa kwanza kupanda jukwaani.
Hadi sasa AY ametoa albamu zake mbili, Raha Kamili (2003) na Hisia Zangu (2005), pamoja na moja ya ushirikiano, Habari Ndio Hiyo (2008) akiwa na Mwana FA, huku akishinda tuzo za muziki Tanzania (TMA), Channel O, Kisima Awards n.k.