IRINGA: Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Richard Kasesela, amesema CCM itaendelea kushinda uchaguzi kutokana na utekelezaji wa miradi ya maendeleo unaofanywa na serikali yake, huku akisisitiza kuwa changamoto kubwa iliyobaki si ukosefu wa kazi, bali ni baadhi ya watumishi wa umma kushindwa kuwahudumia wananchi kwa utu.
Kasesela, ambaye amewahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Iringa na sasa amerejea katika siasa za mkoa huo, alitoa kauli hiyo wakati wa kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Iringa, akisema uzoefu wake wa kuiongoza wilaya hiyo pamoja na ziara za Kamati ya Siasa zimempa nafasi ya kujionea utekelezaji wa Ilani ya CCM ukiwa na matokeo yanayoonekana.
Alisema miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika sekta mbalimbali inaonesha kuwa Serikali inafanya kazi, jambo ambalo linaifanya CCM kuendelea kupata uungwaji mkono wa wananchi.

“Nimejionea miradi. Nina uzoefu kwa sababu nimewahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Iringa. Naona kazi inafanyika vizuri sana. Nakupongeza Mkuu wa Mkoa, Kheri James, kwa kazi kubwa mnayoifanya,” alisema.
Hata hivyo, alisema mafanikio hayo yanapaswa kuambatana na huduma zenye utu kutoka kwa watumishi wa umma, akieleza kuwa wananchi hawapimi maendeleo kwa miradi pekee, bali pia kwa namna wanavyopokelewa na kutatuliwa changamoto zao wanapofika katika ofisi za Serikali.
“Tumepewa mambo mawili tu; kazi na utu. Kazi mnafanya vizuri. Kilichobaki ni utu. Maana ya utu ni kutatua kero za Watanzania,” alisema.
Alisisitiza kuwa huduma zenye heshima, uwajibikaji na usikivu kwa wananchi ndizo zitakazoongeza imani ya wananchi kwa serikali na kukiimarisha chama katika chaguzi zijazo.
Kasesela pia aliipongeza Serikali ya Mkoa wa Iringa pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama kwa kuendelea kudumisha amani, akisema mazingira hayo ndiyo msingi wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo na ukuaji wa uchumi.
Aliwataka viongozi na watumishi wa Serikali kuendelea kuongozwa na falsafa ya 4R ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan ya Maridhiano, Ustahimilivu, Mageuzi na Kujenga Upya, akisema ndiyo dira inayopaswa kuongoza utoaji wa huduma kwa wananchi.
Mbali na hayo, Kasesela aliibua suala la kukamilishwa kwa ujenzi wa kilomita tano za barabara ya Itamba, akisema wakazi wa eneo hilo bado wanakabiliwa na changamoto ya vumbi licha ya ahadi ya utekelezaji wa mradi huo.
Aliiomba Serikali ya Mkoa kufuatilia utekelezaji wa sehemu iliyosalia ya mradi huo ili kuondoa kero kwa wananchi.