RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Hussein Ali Mwinyi, amewataka wahitimu wa Taasisi ya Teknolojia ya India Madras (IIT Madras) kutumia elimu, maarifa na ubunifu wao kama nyenzo za kutatua changamoto za jamii, kuboresha maisha ya wananchi na kuchangia maendeleo endelevu.

Akizungumza katika Mahafali ya 63 ya IIT Madras yaliyofanyika Julai 17, 2026, jijini Chennai, India, Dk. Mwinyi amesema elimu ni msingi muhimu wa kujenga taifa lenye maendeleo kuimarisha jamii na kuandaa kizazi chenye maarifa, ujuzi na uwezo wa kuleta mabadiliko chanya.

Amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kuwekeza katika elimu ya juu, sayansi, teknolojia na ubunifu, akieleza kuwa sekta hizo ni nguzo muhimu katika utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa na Ajenda ya Uchumi wa Buluu.

Rais Mwinyi amebainisha kuwa kuanzishwa kwa Kampasi ya IIT Madras Zanzibar kumefungua ukurasa mpya wa ushirikiano wa kielimu kati ya Tanzania na India. Amesema kampasi hiyo inatoa fursa kwa vijana wa Afrika kupata elimu ya kiwango cha kimataifa huku ikiimarisha utafiti, ubunifu na ujasiriamali.

Katika mahafali hayo, Dk. Mwinyi alishiriki kuwatunuku wahitimu wa ngazi mbalimbali za elimu ya juu, wakiwemo wahitimu wa shahada ya kwanza na shahada ya uzamivu (PhD). Aidha, alitunukiwa Tuzo Maalum kutoka IIT Madras kwa kutambua mchango wake katika kuanzishwa na kuendelezwa kwa Kampasi ya IIT Madras Zanzibar. SOMA: Rais Mwinyi awakaribisha Sweden kuwekeza Zanzibar

Mahafali hayo yaliambatana na uzinduzi wa mradi wa ujenzi wa kampasi mpya ya kudumu ya IIT Madras Zanzibar inayotarajiwa kuimarisha nafasi ya Zanzibar kama kitovu cha elimu ya juu, utafiti, teknolojia na ubunifu katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *