ARUSHA: Ongezeko la idadi ya wagonjwa katika kambi ya matibabu iliyoratibiwa na Waziri wa Habari, Michezo, Sanaa na Utamaduni, ambaye pia ni Mbunge wa Arusha Mjini, Paul Makonda, limeifanya Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kuongeza idadi ya madaktari bingwa na wabobezi wanaotoa huduma katika kambi hiyo.
Akizungumza akiwa kambini, Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Dk. Dalilah Kimambo, alisema mwitikio wa wananchi umekuwa mkubwa siku hadi siku, hali iliyosababisha kuongeza wataalamu ili kuhakikisha wagonjwa wote wanapata huduma kwa wakati.
Alisema kutokana na idadi kubwa ya wagonjwa, huduma zinaendelea hadi usiku kwani eneo la kambi limewekewa taa ili kurahisisha utoaji wa huduma.

“Kutokana na ongezeko hili la wagonjwa, tumeongeza madaktari bingwa na wabobezi ili kuhakikisha katika siku hizi tatu za mwisho wa kambi, wagonjwa wote watakaopewa namba wanapatiwa matibabu bila wasiwasi wowote,” alisema Dk. Kimambo.
Alieleza kuwa wagonjwa wa macho ndio wamekuwa wengi zaidi kuliko wa magonjwa mengine, ambapo kila siku hufanyika upasuaji mdogo na mkubwa kwa wastani wa wagonjwa 47, huku idadi hiyo ikitarajiwa kuongezeka katika siku zilizobaki za kambi.
Aidha, alisema MNH imeongeza wataalamu wa fani mbalimbali ili kukidhi mahitaji ya wananchi wanaofika kupata huduma za kibingwa.
Dk. Kimambo alisema kambi hiyo, iliyoandaliwa na Makonda kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, imekuwa msaada mkubwa kwa wananchi wa Jiji la Arusha na maeneo mengine nchini, huku ikitarajiwa kufanyika kila mwaka.
“Tunapaswa kumpongeza Makonda kwa uamuzi wake wa kuanzisha kambi hii ya matibabu yenye lengo la kuwafikishia huduma za tiba wananchi, hususan wasiokuwa na uwezo. Hili ni jambo jema na linastahili kupongezwa,” alisema Dkt. Kimambo.
Kwa upande wake, Waziri Paul Makonda alimshukuru Dk. Kimambo pamoja na uongozi wa MNH kwa kujitolea kuongeza wataalamu kufuatia mwitikio mkubwa wa wananchi.

Alisema hatua hiyo inaonesha dhamira ya kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora za afya, hususan wale wasiokuwa na uwezo wa kumudu gharama za matibabu.
Makonda pia alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa unaoendelea kufanywa katika sekta ya afya kupitia ununuzi wa vifaa tiba, upatikanaji wa dawa pamoja na programu za kuwajengea uwezo madaktari bingwa na wabobezi ndani na nje ya nchi.
Alisema uwekezaji huo umeongeza imani ya wananchi kwa madaktari wa Kitanzania na umewezesha huduma za kibingwa kuwafikia wananchi kupitia kambi hiyo ya matibabu.

Vilevile, aliwahimiza wananchi waliopangiwa tarehe za kurejea kambini kufika kwa wakati ili kuendelea na matibabu yao, akisisitiza kuwa hakuna mgonjwa atakayekosa huduma katika kipindi chote cha kambi hiyo inayofanyika katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha.