MOROGORO: Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimepongeza Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta ya Binafsi (PPPC) kwa kuendelea kuhamasisha matumizi ya ubia (PPP) kama nyenzo ya kuharakisha maendeleo ya sekta ya kilimo na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Akizungumza leo Julai 17, 2026 wakati wa Mhadhara wa Wazi kwa Umma ulioandaliwa na PPPC katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo, Naibu Makamu Mkuu wa SUA, Prof. Amandus Muhairwa, alisema uamuzi wa PPPC kuandaa mhadhara huo chuoni hapo unaonesha kutambua nafasi ya kimkakati ya kilimo katika kufanikisha ajenda ya maendeleo ya Tanzania.

Alisema SUA imefarijika kuwa miongoni mwa taasisi za elimu ya juu zinazoshirikishwa katika mijadala kuhusu ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi, akibainisha kuwa ushirikiano huo ni hatua muhimu katika kuunganisha elimu, utafiti, ubunifu na uwekezaji kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.

“Tunayo heshima kubwa kumpokea Mkurugenzi Mtendaji wa PPPC, David Kafulila, pamoja na ujumbe wake. Uamuzi wa kuja SUA hauoneshi tu dhamira ya kuendeleza ajenda ya ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi, bali pia unaakisi utambuzi wa nafasi ya kimkakati ya kilimo katika kuharakisha mabadiliko ya kiuchumi nchini,” alisema Prof. Muhairwa.

Alisisitiza kuwa maendeleo ya kilimo ndiyo msingi wa mafanikio ya sekta nyingine za uzalishaji na kwamba uwekezaji kupitia ubia una nafasi kubwa ya kuongeza tija, kuimarisha mnyororo wa thamani wa mazao, kuchochea ukuaji wa viwanda vinavyotegemea malighafi za kilimo na kuongeza ajira.

“Bila kilimo hakuna viwanda, hakuna ajira. Kilimo ndicho msingi wa uchumi wetu. Tukikiwekea mazingira bora ya uwekezaji kupitia ushirikiano wa Serikali, sekta binafsi na taasisi za utafiti, tutafungua fursa nyingi zaidi za ukuaji wa uchumi na ustawi wa wananchi,” alisisitiza.

Aidha, Prof. Muhairwa alisema SUA itaendelea kushirikiana na PPPC katika kuendeleza tafiti, ubunifu na teknolojia zinazoweza kuongeza thamani ya sekta ya kilimo na kuvutia uwekezaji wenye tija kupitia miradi ya ubia.

Mhadhara huo wa wazi ni sehemu ya programu ya PPPC ya kujenga uelewa kuhusu nafasi ya ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Kupitia majukwaa ya aina hii, PPPC inaendelea kuimarisha ushirikiano na taasisi za elimu ya juu, sekta binafsi na wadau wengine wa maendeleo ili kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji na kuharakisha utekelezaji wa miradi yenye manufaa kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.

Ushirikiano kati ya PPPC na taasisi za elimu kama SUA unaendelea kuwa kichocheo muhimu cha kuunganisha maarifa, sera na uwekezaji, hatua inayochangia kuimarisha uchumi unaojengwa juu ya uzalishaji, ubunifu na ushirikiano endelevu kati ya sekta ya umma na sekta binafsi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *