WAKATI Simba Queens ikijiandaa kuingia kambini Julai 19, 2026 kwa ajili ya maandalizi ya michuano ya kufuzu Ligi ya Mabingwa Afrika kwa Ukanda wa Cecafa, mabingwa hao wameanza kufanya maboresho ya kikosi ikielezwa imeachana na kiungo wa Nigeria, Amarachi Odoma.

Kiungo huyo anaondoka Msimbazi baada ya kushindwa kujihakikishia nafasi ya kudumu katika kikosi cha kwanza tangu alipotua mwanzoni mwa msimu wa 2025-2026 akitokea klabu ya Edo Queens ya Nigeria.

Alitua kwa matumaini makubwa, lakini mambo hayakwenda kama alivyotarajia kutokana na ushindani mkubwa uliokuwepo katika safu ya kiungo ya Simba Queens, ambayo msimu uliopita ilikuwa miongoni mwa maeneo yenye wachezaji waliokuwa katika kiwango bora.

Amarachi alikuwa akishindania namba na viungo wengine Elizabeth Joseph, Viviane Corazone na Fasila Adhiambo, ambao walikuwa chaguo la kwanza kwa kocha Mussa Hassan ‘Mgosi’ kutokana na ubora wao katika kuunganisha safu ya ulinzi na ushambuliaji.

Kutokana na hali hiyo, Mnaigeria huyo alishindwa kupata muda wa kutosha wa kucheza katika mechi nyingi.

Mbali na kiungo huyo, pia Simba imeachana na mshambuliaji Jentrix Shikangwa ambaye ametimkia FC Masar ya Misri.

Mratibu wa Simba Queens, Selemani Makanya, amesema ni mpango mkakati wa timu kufanya maboresho machache na kuongeza wachezaji wapya kuelekea kwenye mashindano makubwa ya Afrika.

“Msimu uliopita ulikuwa wa kutengeneza timu na tayari imepata muunganiko, hivyo tumezungumza na kocha Mgosi na ametuelekeza mabadiliko madogodogo tu ya kuyafanya na tayari tumeyafanyia kazi,” amesema Makanya.

Kwa upande wa Mgosi amesema: “Tayari tumemaliza kila kitu kwenye usajili, kilichobaki ni utambulisho tu kama ambavyo mnafahamu imekuwa ikifanywa kwenye kilele cha Simba Day.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *