ZAIDI ya wachezaji 150 wa gofu kutoka ndani na nje ya Tanzania, wanatarajiwa kushiriki mashindano ya Vodacom Corporate Masters 2026 yatakayofanyika Agosti 1, 2026 kwenye Viwanja vya Gofu Lugalo, Dar es Salaam.

Mashindano hayo, yanayodhaminiwa na Vodacom Tanzania Plc kwa kushirikiana na Oakwood Holdings Limited, yatawakutanisha wanaume, wanawake na wachezaji chipukizi kutoka klabu mbalimbali nchini pamoja na mataifa jirani.

Washiriki watashindana kwa mfumo wa stroke play wa mashimo 18, huku timu 10 za makampuni zikichuana kuwania taji la Vodacom Corporate Masters 2026.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mashindano hayo, Mkuu wa Idara ya Masoko na Uwezeshaji wa Vodacom Tanzania Plc, Joseph Sayi, amesema tukio hilo limeendelea kuwa zaidi ya mashindano ya michezo kwa kuwa linatoa fursa ya kuwakutanisha viongozi wa biashara, wabunifu na watoa maamuzi.

“Vodacom tunaamini ukuaji endelevu wa biashara unajengwa kupitia mahusiano imara. Mashindano haya ni jukwaa la kujenga ushirikiano, kubadilishana mawazo na kutafuta fursa mpya zitakazochochea safari ya Tanzania kuelekea uchumi wa kidijitali,” amesema Sayi.

Ameongeza kuwa kupitia Vodacom Business, kampuni hiyo itaonyesha suluhisho mbalimbali za kidijitali ikiwemo huduma za mawasiliano, usalama wa mtandao na teknolojia za biashara zinazosaidia taasisi kuongeza ufanisi na ushindani.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Corporate Masters, Ken Kariuki, amesema mashindano hayo yamekuwa jukwaa muhimu la kuunganisha makampuni, kuongeza thamani ya chapa na kufungua fursa mpya za biashara.

Mbali na ushindani wa gofu, tukio hilo litakuwa na maonesho ya makampuni, burudani mbalimbali, maonesho ya magari na vitu vya kale (vintage) pamoja na eneo maalumu la watoto, hatua inayolenga kuwapa burudani washiriki na familia zao.

Mashindano ya Vodacom Corporate Masters yameendelea kujijengea sifa ya kuunganisha michezo, biashara na ubunifu, huku yakiongeza mchango wake katika kukuza mchezo wa gofu na mahusiano ya kibiashara nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *