
Waziri wa Sheria wa Sudan, Abdullah Darf, amewasilisha kifurushi cha njia za kisheria “zisizo za kawaida” ambazo serikali ya Khartoum inakusudia kuchukua ili kufungua mashtaka dhidi ya serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na kundi la waasi la Rapid Support Forces (RSF), akisisitiza kwamba Khartoum ina “ushahidi wa kutosha na data kamili” kuhusu “ushiriki wa Abu Dhabi katika vita na uhalifu uliofanywa na pande hizo mbili dhidi ya watu wa Sudan.”
Haya yamekuja wakati wa ukaguzi wa maonyesho ya silaha za kisasa na zana za kijeshi zilizokamatwa na Vikosi vya Jeshi la Sudan kutoka kwa waasi wa RSF katika maeneo mbalimbali ya mapigano.
Waziri wa Sheria wa Sudan ameeleza kwamba maonyesho hayo yanajumuisha silaha za kisasa, ikiwa ni pamoja na ndege zisizo na rubani za kimkakati zilizotengenezwa miaka ya 2023, 2024, na 2025.
Abdullah Darf amesisitiza kwamba uchunguzi wa kiufundi na kijinai wa silaha hizo “unathibitisha kwa yakini kwamba mtumiaji wa mwisho aliyesajiliwa rasmi, kwa mujibu wa makubaliano ya biashara ya silaha za kimataifa, ni Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE),” akisisitiza kwamba “uthibitisho huu unaondoa shaka yote kuhusu ushiriki wa moja kwa moja wa Imarati katika kuwapa silaha waasi wa RSF.”
Amesema kwamba “uhalifu unaofanywa dhidi ya watu wa Sudan ni uhalifu wa kivita na jinai dhidi ya ubinadamu zinazofanywa na waasi wa Rapid Support Forces kwa msaada na uwezeshaji wa moja kwa moja wa UAE.” Ameeleza zaidi kwamba “ushahidi tulionao leo unatosha kabisa kuwafungulia mashtaka.”
Waziri wa Sheria wa Sudan pia ameikosoa vikali Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC), akisema Khartoum imekatishwa tamaa na kutochukua hatua kwa mahakama hiyo. Amesema serikali ya Sudan ilikuwa na matumaini kwamba ICC itatoa hati za kukamatwa viongozi wa RSF ambao amewatuhumu kuwa wamefanya mauaji ya halaiki katika miji ya El Geneina na El Fasher na katika jimbo la El Gezira.
Darf ameongeza: “Licha na kuwasilishwa ushahidi wa wazi, mahakama ya ICC bado haijatoa hati za kukamatwa watuhumiwa.”
Mashirika ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu yanaeleza kuwa Imarati (UAE) inahusika katika mzozo wa Sudan kupitia uungaji mkono wa kijeshi na kifedha kwa kundi la wanamgambo wa Rapid Support Forces (RSF), kundi ambalo limetuhumiwa kutenda uhalifu wa kivita na mauaji ya kimbari.
Uchunguzi wa Amnesty International na ripoti za wataalamu wa Umoja wa Mataifa zinaonesha kuwa Imarati imekuwa ikiipatia RSF silaha za kisasa zikiwemo ndege zisizo na rubani, mabomu na magari ya kijeshi yanayosafirishwa kupitia nchi jirani kama vile Chad.