Umoja wa Mataifa umeonya kwamba kusafirisha miili za waathiriwa wa virusi vya Ebola kati ya maeneo mbalimbali kwa ajili ya mazishi katika miji yao kunaweza kuchangia kuenea kwa maambukizi, wakati huu ambapo idadi ya maambukizi ya virusi hivyo imeongezeka kwa takriban 70% katika wiki mbili, huku zaidi ya maambukizi 40 mapya yakirekodiwa kila siku kwa wastani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Shirika la Kimataifa la Uhamiaji limethibitisha kwamba mila na ada za mazishi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo zinaunda mojawapo ya changamoto zinazokabili juhudi za kudhibiti mlipuko huo, kutokana na kuendelea maambukizi ya virusi kupitia njia ya kugusana na miili ya marehemu, jambo linalohitaji kufuata taratibu salama za mazishi.

Mkurugenzi wa Operesheni za Tahadhari na Majibu ya Dharura wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Dkt. Abdul Rahman Mahmoud, amesema kwamba mlipuko wa sasa wa Ebola umekuwa mlipuko wa tatu kwa ukubwa wa Ebola katika historia katika miezi miwili tu na mojawapo ya mlipuko yenye kasi kubwa zaidi, akieleza kuwa zaidi ya visa 2,100 vilivyothibitishwa na zaidi ya vifo 800 vimerekodiwa.

Ameongeza kuwa mgogoro huo umevuka kiwango cha kuwa mlipuko wa janga, kwani unaandamana na hali ngumu ya binadamu na usalama tete katika maeneo yenye migogoro mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ambapo ghasia za kutumia silaha na uhamaji mkubwa wa watu unatatiza juhudi za kukabiliana na kudhibiti ugonjwa huo.

Dkt. Abdul Rahman Mahmoud amesema kwamba virusi vinavyosababisha mlipuko wa sasa ni aina ya Bundibugyo, ambayo kwa sasa haina chanjo au matibabu maalumu, akisisitiza kwamba Shirika la Afya Duniani linaendelea kuunga mkono Wizara ya Afya ya Congo ili kupunguza maambukizi ya ugonjwa huo na kulinda jamii zilizoathiriwa.

Kuhusu usafirishaji wa miili ya wahanga wa Ebola, afisa huyo amefafanua kwamba virusi vya Ebola hutofautiana na magonjwa mengi ya kuambukiza, kwani hubaki kwenye mwili wa marehemu kwa kiwango kikubwa baada ya kifo, na kufanya utunzaji wa mwili na shughuli za mazishi kuwa miongoni mwa hatua hatari zaidi za maambukizi.

Amesema kwamba hii inahitaji kufuata hatua kali za kinga ili kulinda familia za waathiriwa, wafanyakazi wa huduma za matibabu na wale wanaoshiriki katika sherehe za mazishi.

Hapo awali, Shirika la Afya Dunia (WHO) lilitangaza kwamba kwa uchache maambukizo 1,963 yamerekodiwa, ambayo watu wasiopungua 719 wameaga dunia. Baadhi ya ripoti zinasema idadi halisi ya maambukizi ya virusi vya Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo huenda ikawa kwa uchache mara mbili ya idadi rasmi iliyotangazwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *