WAKATI Mbeya City ikiendelea na maandalizi ya msimu ujao wa 2026-2027, imeanza harakati za usajili na kumshusha kikosini hapo mkali wa mabao, Ismail Aziz Kada ambaye kutoka Fountain Gate, huku ikielezwa mastaa wengine kuendelea kutua kikosini.

Wakati sura mpya zikianza kushuka, vigogo wa timu hiyo wamemuhakikishia Kocha Mkuu, Salum Mayanga kuendelea na majukumu yake, huku ikitarajia kuingia kambini muda wowote kujiwinda na msimu ujao.

Mayanga alijiunga na timu hiyo katikati ya msimu uliopita akiziba nafasi ya mtangulizi wake, Malale Hamsini aliyesitishiwa mkataba kutokana na matokeo yasiyoridhisha na kufanikiwa kuibakisha salama timu hiyo.

Usajili wa Kada, unatajwa kwenda kuimarisha kikosi cha Mbeya City kwani nyota huyo alikuwa miongoni mwa vinara wa mabao kwenye kikosi cha Fountain Gate, akifunga mabao matano na asisti tano wakati timu hiyo ikimaliza msimu nafasi ya 12 kwenye ligi na pointi 33.

KAD 01

Mbeya City haikuwa na matokeo mazuri katika msimu uliopita ilipomaliza nafasi ya 13 na kuangukia mtoano ‘play off’ na kufanikiwa kushinda kwa jumla ya mabao 2-0 dhidi ya Tanzania Prisons.

Akizungumza na Mwanaspoti Ofisa Habari wa Mbeya City, Gwamaka Mwankota, amesema usajili huo ni mwanzo wa kusuka kikosi kipya kwa ajili ya msimu ujao, akieleza kuwa nyota wengine wapya wataendelea kuonekana.

Kuhusu idadi inayohitajika kulingana na ripoti na mapendekezo ya benchi la ufundi, Mwankota amesema kanuni inaruhusu wachezaji 40, hivyo muda na mahitaji ya timu ndio itaamua nani aingie au kutoka.

KAD 02

“Kwakuwa bado muda unaruhusu na kanuni inaelekeza kusajili wachezaji 40, bado ni mapema licha ya benchi la ufundi kupendekeza, tutaangalia mahitaji ya timu, lakini huo ni usajili wa kwanza na tutaona wengine,” amesema Mwankota.

Ameongeza kuwa, timu hiyo inatarajia kuingia kambini muda wowote kuanzia sasa baada ya mipango na taratibu kukamilika, akiahidi kuwa na kikosi bora msimu ujao kutokana malengo waliyonayo.

Kwa upande wake Kada ambaye amesaini mkataba wa mwaka mmoja, amesema ndani ya siku nne kuanzia sasa atatua jijini Mbeya kuungana na wenzake tayari kuianza safari ya msimu ujao akitarajia kufanya vizuri zaidi ya msimu uliopita.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *