MABINGWA wa Ligi Kuu Zanzibar 2025-2026, KVZ, wameanza kutambulisha mashine mpya ndani ya kikosi hicho, kwa ajili ya kuongeza nguvu kuelekea msimu wa 2026-2027 ambapo timu hiyo itashiriki mashindano mbalimbali ikiwemo Ligi ya Mabingwa Afrika.

Mashine hizo zilizotambulishwa ni Hamid Bakari Omar ‘Gaucho’, Nature Mwakilembe, Said Mussa ‘Mbeki’ na Agustino Chalamba ‘Kaseke’. Wakati huohuo, KVZ imetangaza kuachana na wachezaji watano ambao ni Juma Shaban, Mussa Majuto, Raphael Lucas, Mussa Jeba na Abdulhalim Pochinki.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kocha Mkuu wa KVZ, Hababuu Ali, amesema uongozi wa klabu hiyo unaendelea kufanya tathmini ya wachezaji mbalimbali. Kocha huyo amesema wachezaji ambao wameshatambulishwa, ndio waliofanikiwa kupita katika majaribio waliyokuwa wanafanyiwa.

“Kwasasa KVZ inalenga kuwa na wachezaji wazuri na wenye uwezo wa kupambana katika mashindano yote tunayotarajia kushiriki,” amesema kocha huyo. Mbali na hilo, amesema benchi la ufundi linaendelea kupitia kikosi kilichopo ili kubaini watakaoendelea na watakaoachwa.

Aliendelea, kusema kuwa wanafanya tathmini ya kila nafasi uwanjani kuhakikisha wanapata wachezaji watakaongeza nguvu. Hivyo, aliwataka wachezaji waendelee kujituma kikosini hapo kwa sababu bado wapo katika mchujo.

Amesema, katika kuhakikisha timu hiyo inakuwa bora, hailengi kufanya usajili kwa pupa badala yake watatafuta wachezaji watakaokidhi mahitaji ya timu. Kikosi hicho tayari kimeingia kambini na kinatarajiwa kushiriki Kombe la Kagame, michuano inayoanza Julai 24 hadi Agosti 7 mwaka huu nchini Rwanda.

KVZ inayoiwakilisha Zanzibar kwenye michuano ya Kagame mwaka huu, imepangwa Kundi C na timu za Al Hilal kutoka Sudan, Rayon Sports ya Rwanda na Tusker ya Kenya. Julai 26, KVZ itaanza kwa kucheza dhidi ya Rayon Sports, kisha Al Hilal (Julai 29), itahitimisha makundi ikiikabili Tusker (Agosti 1).

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *