Mwanaharakati na mhandisi wa India, Sonam Wangchuk amelazwa hospitalini mjini New Delhi baada ya polisi kumhamisha kwa nguvu kufuatia mgomo wa njaa wa siku 20 uliokuwa ukihatarisha afya yake.

Wangchuk, mwenye umri wa miaka 59, alianza mgomo huo Juni 28 akitaka Waziri wa Elimu, Dharmendra Pradhan, ajiuzulu kutokana na madai ya kasoro na udanganyifu katika mfumo wa mitihani ya kujiunga na masomo ya udaktari. Polisi walisema hatua hiyo ilichukuliwa kwa kufuata maagizo ya Mahakama Kuu ya Delhi na ushauri wa madaktari waliokuwa wakifuatilia hali yake.

Kumhamisha Wangchuk kulizua msukosuko katika eneo la maandamano la Jantar Mantar, ambako mamia ya wanafunzi walikuwa wakimuunga mkono. Video kutoka eneo hilo zilionyesha polisi wakimbeba Wangchuk kutoka jukwaani huku baadhi ya waandamanaji wakijaribu kuzuia zoezi hilo. Mke wake, Gitanjali J. Angmo, alisema yupo pamoja naye hospitalini na kusisitiza kuwa hakuna matibabu yanayopaswa kutolewa bila idhini ya familia na madaktari waliokuwa wakimsimamia tangu alipoanza mgomo.

Zaidi ya wanafunzi milioni 2.2 waliolenga kujiunga na masomo ya udaktari walilazimika kufanya upya mtihani wa NEET baada ya mtihani wa awali kufutwa kutokana na kuvuja kwa maswali. Sakata hilo, pamoja na hitilafu nyingine katika mitihani ya shule za sekondari, limechochea maandamano ya vijana kote nchini.
Baada ya Wangchuk kupelekwa hospitalini, mwanzilishi wa chama cha Cockroach Janta Party (CJP), Abhijeet Dipke, alitangaza kuanza mgomo wa njaa usio na kikomo akidai serikali imefanya kosa kubwa. Mahakama Kuu ya Delhi ilikuwa tayari imeelekeza kuwa maisha ya Wangchuk yalindwe kwa gharama yoyote na kwamba apatiwe matibabu yote muhimu.

Wangchuk, anayefahamika kimataifa kwa ubunifu wake katika miradi ya uhifadhi wa maji katika milima ya Himalaya, alisema muda mfupi kabla ya kuhamishwa hospitalini kuwa hata harakati ndogo zinaweza kuleta mabadiliko makubwa ya kisiasa nchini India, hasa pale zinapolenga kuboresha elimu.

#AzamTVUPdates
Mhariri | John Mbalamwezi

(Feed generated with FetchRSS)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *