DAR ES SALAAM: Ubunifu wa Saratani AI na Dawa Mkononi ni miongoni mwa miradi iliyoanzia katika tukio la Winning Line Academic Event la Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), ambayo sasa imeendelea kutoa suluhisho kwa wananchi ndani na nje ya Tanzania.

Ubunifu huo umetajwa kuwa sehemu ya mafanikio ikitoa nafasi kwa wanafunzi wa MUHAS na vyuo mbalimbali vya afya nchini kuwasilisha tafiti, kushindanisha bunifu na kujenga mitandao ya ushirikiano wa kitaaluma.

Akizungumza katika maadhimisho ya miaka 20 ya jukwaa hilo tangu kuanzishwa mwaka 2006, Mgeni Rasmi, Marsha Macatta Yambi, Makamu Mwenyekiti wa Baraza la MUHAS na Rais wa Jumuiya ya Wahitimu wa MUHAS (MUHAS Convocation), amesema jukwaa hilo limezalisha wabunifu wengi ambao mawazo yao yamekua na kuwa suluhisho halisi katika sekta ya afya.

Ametaja ubunifu wa Saratani AI na Dawa Mkononi kuwa miongoni mwa miradi iliyoanzia kwenye jukwaa hilo na sasa imeendelea kutumika kutoa suluhisho kwa wananchi ndani na nje ya Tanzania.

Dk. Makata alisema mwaka huu jukwaa limepokea zaidi ya bunifu 100 zenye thamani ya takribani Sh milioni 27, huku akitoa wito kwa sekta binafsi na wadau mbalimbali kushirikiana na wanafunzi ili kuendeleza ubunifu huo.

“Tunataka mawazo ya wanafunzi yasibaki maktabani. Yahitaji kuungwa mkono ili yawe suluhisho kwa jamii na kuchangia maendeleo ya sekta ya afya nchini na duniani,” amesema.

Kwa upande wake, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu (DVC-RC), Profesa Bruno Sunguya, amesema Winning Line limekuwa msingi wa kuwajenga watafiti wengi wanaoongoza sekta ya afya nchini.
Amesema viongozi na watafiti wengi wanaotambulika leo waliwahi kushiriki katika jukwaa hilo walipokuwa wanafunzi, jambo linaloonyesha mchango wake katika kukuza vipaji vya utafiti.

“Jukwaa hili linawajenga wanafunzi kuwa watafiti mahiri, linawapa ujasiri wa kushindana, kujenga mitandao ya ushirikiano na kuwafundisha namna ya kuandika miradi ya utafiti na kutafuta fedha,” amesema.

Ameongeza kuwa wanafunzi wanapaswa kuelekeza nguvu zaidi katika matumizi ya teknolojia na kufanya tafiti zinazolenga changamoto zinazoibuka kwa kasi, hususan magonjwa yasiyoambukiza kama kisukari, shinikizo la damu, saratani na magonjwa ya afya ya akili.

Naye mwanafunzi wa mwaka wa tano wa udaktari MUHAS, Emmanuela Maira, amesema jukwaa hilo limemwezesha kuwasilisha utafiti wake unaochunguza athari za dalili zinazowakabili wanawake kabla ya hedhi katika masomo na shughuli za kila siku.

Amesema kupitia Winning Line amepata nafasi ya kukutana na wataalamu mbalimbali wanaoweza kumsaidia kuendeleza utafiti wake hadi uweze kutumika katika kuboresha sera za afya.

Kwa upande wake, Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Afya KCMC, Erick Mahatara, amesema jukwaa hilo limewapa wanafunzi fursa ya kujifunza, kujenga uzoefu na kuanzisha ushirikiano wa kitaaluma utakaowasaidia kuwa watafiti wakubwa siku zijazo.


Amesisitiza kuwa tafiti za kisasa zinahitaji ushirikiano wa taaluma mbalimbali, hivyo majukwaa kama Winning Line yanawawezesha wanafunzi kuanzisha mtandao wa wataalamu mapema kabla ya kuingia rasmi kwenye taaluma zao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *