SIMBA inaendelea na hesabu za kusuka kikosi chake na sasa kuna mashine mbili kutoka Mali zinakuja kuangaliwa na kocha Steve Barker kabla ya kupewa mikataba ya miaka miwili kila mmoja kuvaa jezi nyekundu na nyeupe.

Simba ambao ni mabingwa wa Kombe la CRDB wanaboresha kikosi chao kwa ajili ya kufanya vizuri msimu ujao, kuanzia kwenye michuano ya Kagame Cup, Ngao ya Jamii, Kombe la CRDB Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo timu hiyo itashiriki.

Kuonyesha kuwa ipo kwenye mikakati bora jana ilimtambulisha kiungo Kelvin Nashon kutoka Pamba ambaye katikati ya msimu uliopita aliripotiwa na Mwanaspoti kuwa amejiunga na Simba kwa mkataba wa miaka miwili.

Hesabu hizo zinamshusha nchini mshambuliaji Ibrahima Doumbia ambaye ndiye mfungaji bora nchini Mali msimu uliopita, akifunga mabao 17, Simba imeshafanya mazungumzo na staa huyo lakini inataka kocha Barker ajiridhishe kwanza.

Barker hamjui sawasawa Doumbia na ameomba mshambuliaji huyo aje kisha acheze mashindeano ya Kagame ambayo Simba itashiriki kisha kupima ubora wake kabla ya maamuzi ya mwisho ya kupewa mkataba wa miaka miwili.

Bosi wa juu wa Simba ameliambia Mwana spoti kuwa Doumbia ambaye alitangazwa kuwa mchezaji bora wa ligi ya Mali anakuja kutoka kwenye mapendekezo ya maskauti wanaofanya kazi na klabu hiyo ambaye pia alikuwa anawindwa na Al Hilal ya Sudan.

“Tumeambiwa ni mshambuliaji mzuri lakini sisi hatufanyi maamuzi ya mwisho rekodi zake zinashawishi, tunataka kocha wetu (Barker) naye ajiridhishe kama ni mtu anayemtaka, kwa mipango yake, kwa hiyo kuna mambo tumekubaliana na klabu yake na wasimamizi wake,”amesema bosi huyo wa juu kwenye bodi ya Simba.

“Atakuja tutampa nafasi ya kucheza mashindano ya Kagame, kama kocha akijiridhisha kwamba kiwango chake ni kizuri basi tutasaini mkataba wa miaka miwili atakuwa mchezaji wa Simba, tunataka kufanya mambo kwa uhakika zaidi.

Mbali na Doumbia pia safari hiyohiyo itamleta kiungo wa Real Bamako Mohammed Sangare ambaye naye atapewa nafasi kama ya mshambuliaji huyo.

Sangare ambaye anacheza kiungo wa ulinzi anahesabika kama mchezaji mwenye kipaji kikubwa ambapo Simba inataka kumuongeza kuboresha eneo lao la kiungo.

“Hata huyo Sangare naye anakuja kwa njia hiyohiyo, tumeona ni kijana mdogo mwenye kipaji lakini naye kocha hamjui, tunataka ampe nafasi yeye ( Barker) na sisi tutaona kama ni mchezaji mzuri atatufaa basi tutamalizana naye.”

Ujio wa Sangare utakuwa ni presha nyingine kwa Alassane Kante ambapo inaelezwa kama kiwango chake kitawashawishi pande hizo mbili kunaweza kuweka mashakani nafasi ya raia huyo wa Senegal ambaye ametumikia nusu ya mkataba wake wa miaka miwili.

Mashindanio ya Cecafa yataanza Julai 24 nchini Rwanda jijini Kigali ambapo Simba imepangwa kundi B sambamba na timu za Jamus (Sudan), Mogadishu (Somalia)  na Singida Black Stars ambapo pia wekundu hao watatumia nafasi hiyo kuweka kambi ya maandalizi ya msimu mpya.

Akizungumza kuhusu mipango ya msimu ujao, kocha wa Simba, Steve Barker, amesema moja ya maeneo ambayo yeye na uongozi wa klabu walikubaliana kuyaimarisha katika dirisha hili la usajili ni nafasi ya mshambuliaji wa kati.

“Baada ya tathmini ya msimu tulikubaliana kuwa tunahitaji kuongeza ubora katika baadhi ya maeneo. Moja ya nafasi hizo ni mshambuliaji wa kati ili kuongeza ushindani na kuwa na chaguo zaidi ndani ya kikosi,” amesema Barker.

Kauli hiyo inaendana na harakati zinazodaiwa kufanywa na Simba za kumfuatilia Doumbia ambaye pia anatolewa macho na klabu za Afrika Kusini na nyingine zikiwa za ukanda huo.

Akizungumza na Mwanaspoti, mchambuzi wa soka wa Mali, Mamadou Sidibé, amesema Doumbia ni mshambuliaji anayejitofautisha kwa uwezo wake wa kusoma mchezo na kutengeneza nafasi hata akiwa hana mpira.

“Doumbia ni mshambuliaji anayejua kusoma mchezo vizuri, mikimbio yake bila mpira huwafanya mabeki washindwe kujipanga na mara nyingi humkuta akiwa katika nafasi sahihi ya kufunga,” amesema Sidibé.

Mchambuzi huyo amesema silaha nyingine ya mshambuliaji huyo ni utulivu wake anapokuwa ndani ya eneo la hatari, akieleza kuwa hutumia nafasi chache kupata mabao.

“Ni mchezaji mwenye utulivu mkubwa kwenye umaliziaji, ana uwezo wa kufunga kwa miguu yote miwili na pia ni mzuri kwenye mipira ya juu,”.

Kwa mujibu wa Sidibé, Doumbia pia anafahamika kwa uwezo wake wa kuanzisha presha kwa mabeki wa wapinzani, jambo linalosaidia timu yake kurejesha umiliki wa mpira haraka.

“Anapenda kukaba kuanzia mbele. Hiyo ni sifa ambayo kila kocha anayependa mpira wa kasi huifurahia kwa mshambuliaji wake,” amesema.

Mahitaji ya Simba ya kupata mshambuliaji mpya yalionekana wazi mwishoni mwa msimu uliopita baada ya kukumbwa na changamoto katika eneo hilo.

Kusimamishwa kwa Jonathan Sowah kulilazimisha benchi la ufundi kumtumia kiungo mshambuliaji, Elie Mpanzu kucheza kama mshambuliaji wa kati katika baadhi ya mechi muhimu za mwisho wa msimu ili kuziba pengo lililoachwa.

Sowah tayari amerejea Singida Black Stars baada ya kuachana na Simba kufuatia kile kilichoelezwa kuwa ni utovu wa nidhamu, hali iliyoongeza umuhimu wa klabu hiyo kutafuta mshambuliaji mwingine.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *