
Dar es Salaam. Kulwa Maduhu, mmoja wa mawakili wa mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu amedondosha machozi kizimbani wakati akitoa ushahidi wa kuzuiwa kumuona Lissu mahabusu.
Katika ushahidi wake Maduhu ambaye ni mtu mwenye ualibino amedai alizuiwa na ofisa wa Jeshi la Magereza Ukonga kuonana na Lissu kwa sababu ya ualibino wake kwa namna isiyo ya moja kwa moja.
Ametoa maelezo hayo wakati akihojiwa na Lissu maswali mbalimbali ya dodoso kuhusiana na madai yake katika kesi aliyoifungua na wenzake wawili, Mahakama Kuu, Masjala Kuu Dodoma.
Kesi hiyo ya Kikatiba namba 7300/2026 imefunguliwa na wakili Maduhu, Nashon Nkungu na Paul Kisabo, dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Kamishna Mkuu wa Magereza (CGP), Mkuu wa Gereza la Ukonga jijini Dar es Salaam na Lissu mwenyewe.
Hata hivyo, baadaye Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) nacho kiliomba na kikakubaliwa kuunganishwa kwenywe kesi hiyo kama mdaawa mwenye masilahi.
Katika kesi hiyo mawakili hao wanapinga vikwazo wanavyowekewa na mkuu wa Gereza la Ukonga, kila wanapokwenda gerezani kuzungumza na mteja wao, Lissu, anayehifadhiwa katika mahabusu ya gereza hilo kutokana na kesi ya uhaini inayomkabili.
Wadai hao wanajitambulisha washauri wa kisheria wa Lissu, wanalalamikia matendo ya mdaiwa wa tatu (Mkuu wa Gereza Ukonga) kushindwa kutekeleza kanuni ya 13 ya Kanuni za Magereza inayotoa haki ya washauri wa kisheria kufanya mashauriano ya siri na wateja wao bila kuingiliwa.
Maduhu anadai kwa nyakati tofauti wamekuwa wakizuiliwa na maofisa magereza kukutana na kushauriana na Lissu au kumpelekea nyaraka muhimu zinazohusiana na kesi inayomkabili. huku Mkuu wa Gereza akidai ni maelekezo ya Kamishna Mkuu wa Magereza.
Kwa upande wao, Nkungu na Kisabo licha ya kupata fursa ya kuzungumza na kujadiliana na Lissu masuala ya kisheria, lakini wamekuwa hawana faragha kwani maofisa magereza wamekuwa wakisimama umbali wanaoweza kusikia kila kitu wanachojadiliana.
Pamoja na nafuu nyingine wanaiomba mahakama itamke maofisa magereza kusikiliza mazungumzo yao na mteja wao Lissu ni kinyume cha kanuni ya 13 ya Kanuni za Magereza, Sheria na Katiba kuhusu haki ya kusikilizwa kwa usawa na faragha na wapewe fursa ya faragha na mteja wao.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali aliibua pingamizi la awali akidai kuwa kesi hiyo ni batili, kwa kuwa wadai wana njia mbadala za kupata nafuu (wanazoziomba) na hivyo inakiuka kifungu cha 8(2) cha Sheria ya Utekelezaji wa Haki za Msingi na Wajibu (Bradea).
Jopo la majaji watatu wanaosikiliza kesi hiyo, Amir Mruma (kiongozi wa jopo), Dk Angelo Rumisha na Dk Everist Longopa, lilipendekeza pingamizi hilo lisikilizwe kwa pamoja na hoja za kesi ya msingi.
Hata hivyo, Lissu aliomba wadai (waliofungua kesi hiyo) na mdaiwa wa tatu, Mkuu wa Gereza la Ukonga wafike mahakamani awahoji maswali ya dodoso.
Mahojiano hayo yameanza kufanyika leo Jumatatu, Julai 20, 2026 wakati Mahakama hiyo ilipoketi Dar es Salaam kwa ajili hiyo.
Katika mahojiano hayo, Lissu ameanza kumhoji wakili Maduhu.
Kwa mujibu wa mahojiano mara ya kwanza Maduhu alizuiwa gerezani hapo kuonana na Lissu kwa madai kuwa jina lake halikuwemo katika orodha ya mawakili na watu wengine walioorodheshwa na Lissu kumuona gerezani hapo.
Ingawa hata baada ya Lissu kuandika orodha nyingine na kuingiza jina la Maduhu na mawakili wengine ambao hakuwa amewaandika bado alizuiliwa na hata mara ya tatu pia alizuiliwa huku mawakili wengine hata ambao hawakuwepo katika hiyo orodha wakiruhusiwa isipokuwa yeye tu.
Lissu alipomuuliza kama katika mawakili wake wote ni yeye pekee aliyezuiwa Maduhu amejibu ni sahihi huku akisema siku mojawapo wakili mwenzake waliyekwenda pamoja aliruhusiwa lakini yeye akaambiwa aondoke kwa kuwa hayuko kwenye orodha.
“Je, kuna Wakili mwingine ameandikiwa maoni ya namna hiyo kwenye orodha ya mawakili wangu kuwa asinione hayupo kwenye majina niliyompa Bwana Jela,” ameuliza Lissu.
Maduhu: Hakuna wakili mwingine.
Lissu: Je, kuna utaratibu wa kisheria kuhusu mambo haya?
Maduhu: Nimekutana nao Ukonga. Haujawahi kuwepo utaratibu kama huu.
Lissu: Kwani wewe una makosa gani ya Bwana Jela wa Ukonga?
Maduhu: Sifahamiani naye sijui nilichomkosea.
Lissu: Wakati umeruhusiwa kuja kuniona Juma Mwaibako ndio alikuwa anakaimu ukuu wa gereza?
Wakili Maduhu: Ndio
Lissu: Huyu aliyekuzuia ni Andrew Shabani?
Maduhu: Ni sahihi kabisa.
Lissu: Wewe una tatizo la ngozi? albinism?
Maduhu: Sahihi.
Lissu: Kwenye hili Taifa kuna ubaguzi wa watu wenye albinism?
Maduhu: Ni sahihi kabisa.
Lissu: Sasa Wakili aliyezuiwa ni wewe mwenye albinism?
Maduhu: Ni mimi peke yangu ndio nimekataliwa, kwa hiyo nimebagiliwa by implication (kwa namna isiyo ya moja kwa moja)
Lissu: Kwani wewe ulipenda uwe albino?
Maduhu: Sikupenda, ila ndio nimebaguliwa hivyo (huku akiinama na kutokwa machozi).
Hata hivyo, alipohojiwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Stanley Kalokola pamoja na mambo mengine kama maelezo hayo ya kubaguliwa kwa sababu ya ualibino ameyaeleza katika maelezo yake maandishi, amejibu hajayaandika.
Kesi hiyo itaendelea kesho, Jumanne, Julai 21 ambapo Lissu ataendelea kuwahoji wadai wengine kabla ya kuhojiwa na mawakili wengine katika kesi hiyo.