
Dar es Salam. Ndoa ni moja ya uamuzi mkubwa ambao mtu hufanya katika maisha yake.
Hata hivyo, katika jamii nyingi bado kuna mtazamo kwamba ndoa ni hatua inayopaswa kufikiwa kwa sababu ya umri, shinikizo la jamii au mahitaji ya kihisia.
Mtazamo huo umesababisha watu wengi kuingia katika ndoa ambazo baadaye hugeuka kuwa chanzo cha majuto badala ya furaha.
Kwa hakika, msingi wa ndoa yenye mafanikio haupaswi kuwa hisia pekee, bali uhusiano kati ya malengo ya maisha ya wahusika na mwelekeo wa familia wanayotaka kuijenga. Ndoa inapaswa kuwa jukwaa la kukuza ndoto na maono, si mahali pa kuyazika.
Wataalamu wa uhusiano wamekuwa wakisisitiza kwamba mtu anapaswa kujiuliza kama mwenza anayemtaka anaunga mkono malengo yake ya maisha.
Ikiwa baada ya miaka mitatu au minne ya ndoa hakuna maendeleo ya kiuchumi, kitaaluma au hata kimtazamo, kuna uwezekano kwamba wanandoa hawakuwa na dira ya pamoja tangu mwanzo. Ndoa yenye afya huongeza nguvu za kila mmoja na kufungua fursa mpya badala ya kuzifunga.
Ndiyo maana mazungumzo kuhusu ndoto, maono na mipango ya maisha yanapaswa kuanza mapema, hata katika hatua ya urafiki au uchumba.
Kupendana pekee hakutoshi; ni muhimu pia kujua kama maono ya wawili hao yanaendana au yanakinzana. Kukwepa mazungumzo hayo kwa hofu ya kuharibu uhusiano, kunaweza kuzaa migogoro mikubwa baadaye.
Pamoja na hilo, sababu zinazowasukuma watu wengi kuingia kwenye ndoa ndizo zinazostahili kuhojiwa kwa kina. Miongoni mwa makosa makubwa ni kufunga ndoa kwa matarajio ya kupata msaada wa kifedha au kijamii.
Ndoa si taasisi ya kutatua utegemezi, bali ni ushirikiano wa watu wawili wanaojenga maisha kwa pamoja. Anayeingia kwenye ndoa akiwa anatarajia kuokolewa na mwenza wake, anaweza kujikuta akikatishwa tamaa pale matarajio hayo yasipotimia.
Sababu nyingine inayowafanya wengi kufanya uamuzi wa haraka ni umri. Kwa wanawake, shinikizo la kijamii limejenga imani kwamba kuchelewa kuolewa ni kushindwa. Hali hiyo huwafanya baadhi yao kupuuza vigezo vya msingi vya mwenza na kukubali ndoa kwa sababu muda unaonekana kuwatupa mkono.
Ukweli ni kwamba ukomavu wa akili na hisia haupimwi kwa idadi ya miaka. Mtu anaweza kuwa na umri mkubwa lakini bado akakosa uwezo wa kubeba wajibu wa ndoa.
Kadhalika, upweke ni sababu nyingine ambayo mara nyingi huchanganywa na hitaji la kuwa na mwenza. Kuna tofauti kati ya kuwa peke yako na kuwa mpweke.
Upweke ni hali ya ndani ya hisia, wakati kuwa peke yako ni mazingira ya nje. Mtu anaweza kuwa ameoa au ameolewa lakini akaendelea kujisikia mpweke ikiwa hakupata mwenza anayemwelewa na kushirikiana naye. Hivyo, ndoa si dawa ya kutibu upweke wa kihisia.
Shinikizo kutoka kwa wazazi, ndugu au marafiki pia limeendelea kuwa sababu inayowasukuma baadhi ya vijana kuingia kwenye ndoa bila utayari wa kutosha.
Wengine huamua kuoa au kuolewa kwa sababu marafiki wote wamefanya hivyo, huku wakisahau kwamba kila mtu ana safari yake ya maisha. Ukweli unabaki kuwa wanaobeba matokeo ya ndoa si wazazi wala marafiki, bali wanandoa wenyewe.
Aidha, wapo wanaoingia kwenye ndoa wakiamini kwamba ndiyo njia ya kujinasua kutoka katika ukali wa wazazi au mazingira ya nyumbani. Lakini ndoa si tiketi ya uhuru wa kukimbia changamoto za familia.
Mtu anayekimbia tatizo moja bila maandalizi anaweza kujikuta ameingia katika changamoto kubwa zaidi kuliko ile aliyokuwa akiikwepa.
Sababu nyingine inayozua mjadala mkubwa ni kuingia kwenye ndoa kwa sababu ya ujauzito au mtoto. Ingawa mtoto anahitaji malezi ya wazazi wote wawili, hilo pekee halitoshi kuwa msingi wa kujenga ndoa. Pale ambapo hakuna upendo wa kweli, heshima na maono ya pamoja, ndoa inayofungwa kwa kulazimishwa na ujauzito, inaweza kuwa chanzo cha migogoro ya kudumu ambayo huathiri hata ustawi wa mtoto mwenyewe.
Mwisho wa yote, ndoa haipaswi kuwa mwisho wa safari ya ndoto za mtu, bali mwanzo wa hatua mpya ya mafanikio. Mwenza sahihi ni yule anayechochea ukuaji wa mwenzake, anayeheshimu maono yake na kushiriki kuyafanikisha. Kabla ya kusema “ndiyo”, kila mmoja anapaswa kujiuliza swali moja muhimu: Je, ndoa hii itanifanya nikue au itanifanya nipoteze mwelekeo wa maisha yangu?
Jibu la swali hilo linaweza kuwa tofauti kati ya ndoa inayojenga maisha na ndoa inayovunja ndoto.