Dar es Salaam. Imetimia miaka mitatu tangu Bongofleva kutajwa kuwa miongoni mwa aina za muziki wa Afrika utakaopata nafasi ya kuwania Grammy, tuzo zenye hadhi ya juu zaidi duniani katika muziki lakini bado fursa hiyo haijatumika vizuri.
Mnamo Juni 2023, waandaji wa tuzo za Grammy, Recording Academy walitangaza kuanzishwa kwa kipengele kitakachojumuisha aina mbalimbali za muziki kutokea Afrika kiitwacho Best African Music Performance.
Hata hivyo, tangu wakati huo hakuna mwanamuziki kutokea katika Bongofleva ambaye kazi yake imefanikiwa kupata nafasi katika kipengele hicho huku wasanii kutokea Nigeria na Afrika Kusini wakionekana kufanya vizuri.
Mbali na Bongofleva, aina nyingine za muziki zinazozingatiwa katika kipengele hicho ni Afrobeat, Afro-fusion, Afro pop, Afrobeats, Alte, Amapiano, Genge, Kizomba, Chimurenga, High Life, Fuji, Kwassa, Ndombolo, Mapouka, Ghanaian Drill, Hip Hop, Ethio Jazz, Afro-house n.k.
Utakumbuka tuzo za Grammy ambazo ndizo zenye hadhi ya juu kabisa katika tasnia ya muziki duniani, zilianza kutolewa Mei 4, 1959, wakati huo zikifahamika kama Gramophone. Lengo lake kuu ni kutambua na kusherehekea mafanikio ya tasnia ya muziki.
Mwimbaji kutokea Afrika Kusini, Tyla ndiye alikuwa msanii wa kwanza kushinda kipengele cha Best African Music Performance, ni katika msimu wa 66 wa Grammy ambao kwa mara ya kwanza ulitoa fursa hadhimu kwa muziki kutokea Afrika ikiwemo Bongofleva.
Tyla alishinda Grammy 2024 kupitia wimbo wake, Water (2023) akiwabwaga washindani wake ambao ni Asake & Olamide (Amapiano), Burna Boy (City Boys Miracle), Davido ft. Musa Keys (Unavailable) na Ayra Starr (Rush).
Waliowania kipengele hiki ni Tyla pekee ndiye alikuwa hatokei Nigeria, hiyo ndio sababu ushindi wake ulipelekea mashabiki wa nchi hiyo kulalamika sana mtandaoni wakiamini kuwa Davido ndiye alistahili kushinda.
Msimu wa 2025, staa wa Nigeria, Tems akashinda kupitia wimbo wake, Love Me Jeje (2024) mbele ya Asake & Wizkid (MMS), Burna Boy (Higher), Yemi Alade (Tomorrow) na Chris Brown ft. Davido & Lojay (Sensational).
Hiyo ilikuwa Grammy ya kwanza kwa Tems kushinda kupitia kazi yake binafsi, ila ya pili kwa ujumla baada ya hapo awali kushinda kupitia wimbo aliyoshirikishwa na rapa wa Marekani, Future, Wait For U (2022).
Kwa matokeo hayo, Tems aliweka rekodi kama msanii wa kwanza wa kike Nigeria kushinda Grammy, na wa pili baada ya Burna Boy kushinda 2021 kupitia albamu yake ya tano, Twice As Tall (2020). Hawa wawili wameshinda kupitia kazi zao binafsi.
Msimu wa 68, yaani Grammy 2026 ambao ndio wa mwisho kufanyika, wasanii wa Bongofleva wengi waliwasilisha kazi zao katika mchakato wa kupata uteuzi ambapo wengi waliomba kuwania kipengele kile kile cha Best African Music Performance.
Baadhi ambao kazi zao zilithibitishwa kupitia mchujo wa awali ni Marioo (Nairobi), AY (Wanganeka & Simuoni), Fid Q (Glory 2), Diamond Platnumz & Ciara (Low), Abigail Chams (Me Too), huku Harmonize akiingiza nyimbo nne.
Hata hivyo, baada ya kazi hizo kupitiwa, hakuna msanii hata mmoja wa Bongofleva aliyepata nafasi badala yake sura zile zile ndizo zilirejea tena katika kipengele kile maalum kwa ajili ya muziki wa Afrika.
Mchakato huo husimamiwa na waratibu na waandaaji wa tuzo za Grammy, Recording Academy pamoja na wanachama wao ambapo kuzipitia nyimbo zote kisha kuzipigia kura zile zilizokidhi vigezo vya kupata nafasi ya uteuzi.
Ikumbukwe wanachana wa Recording Academy, ni kundi la watu wenye uelewa mkubwa wa muziki wakiwamo wasanii, watunzi wa nyimbo, watayarishaji na wahandisi ambao hupita mchakato maalamu kabla ya kupata nafasi hiyo.
Wakati Bongofleva ikikosa nafasi hiyo kwa msimu wa tatu, waliotajwa kuwania Best African Music Performance katika Grammy 2026, ni Burna Boy (Love), Davido (With You), Hope & Love (Eddy Kenzo), Ayra Starr (Gimme Dat), na Tyla (Push 2 Start) aliyeibuka mshindi ikiwa ni mara ya pili.
Hivyo tangu Afrika kutambulika Grammy miaka mitatu iliyopita, bado wasanii wa muziki huo hawajafanikiwa kufua dafu, huku wanamuziki wa kike (Tyla na Tems) wakiwa ndio pekee walioshinda kipengele cha Best African Music Performance hadi sasa.
Ikumbukwe hadi sasa wasanii wa Afrika walioshinda Grammy kupitia kazi zao wenyewe ni Miriam Makeba (Afrika Kusini) 1966, Sade Adu (Nigeria) 1986, Ali Farka Toure (Mali) 1994, Cesaria Evora (Cape Verde) 2004, Youssou N’Dour (Senegal) 2005.
Wengine ni Angelique Kidjo (Benin), RedOne (Morocco) 2010, Tinariwen (Mali) 2012, Burna Boy (Nigeria) 2021, Black Coffee (Afrika Kusini) 2022, Tyla (Afrika Kusini) 2024 na Tems (Nigeria) 2025.
Angelique Kidjo ambaye amemshirikisha Diamond Platnumz katika wimbo wake, Kakua (2026), ndiye anashikilia rekodi ya kuwa mwanamuziki wa Afrika aliyeshinda tuzo nyingi za Grammy kwa muda wote ambapo ameshinda mara tano.
Lakini haikuwa rahisi kwa Angelique Kidjo kufikia mafanikio hayo kwani mwaka 1983 alilazimika kuondoka Benin kutokana na migogoro ya kisiasa na kuhamia Paris, Ufaransa aliposomea muziki katika Chuo cha CIM.
Katika chuo hicho alikutana na mwanamuziki na mtayarishaji kutokea Ufaransa, Jean Hebrail ambaye walishirikiana katika muziki kabla ya kufunga ndoa mwaka 1987 na kujaliwa mtoto mmoja, Naima aliyezaliwa 1993.
Mwaka 1995, Angelique Kidjo alirejea kwao Benin akiwa na mume wake, Hebrail na kuzunguka sehemu kubwa ya nchi hiyo wakirekodi vionjo vya asili ambavyo vilitumika katika albamu yake ya nane, Fifa (1996).
Baada ya kufanya muziki kwa miaka mingi sana, hatimaye Angelique Kidjo alikuja kushinda tuzo yake ya kwanza ya Grammy kupitia albamu yake ya nane, Djin Djin (2007) iliyoshinda Grammy 2008 kama Albamu Bora ya Muziki Duniani, ikiwa ni takribani miaka 25 tangu alipoanza.