Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Mojtaba Khamenei amesema ukiukaji wa mara kwa mara wa Marekani wa Mkataba wa Maelewano wa Islamabad (MoU) umethibitisha tena kwamba sahihi ya rais wa Marekani “haina thamani kabisa na ni batili.”

Katika ujumbe wake uliotolewa jioni ya jana Jumamosi, Ayatullah Mojtaba Khamenei alisisitiza kwamba vitendo vya Marekani vimefichua kwamba “unyanyasaji, utawala wa mabavu na ukatili” ni vipengele visivyoweza kutenganishwa na tabia na mwenendo wa Marekani.

“Leo, Shetani Mkuu amefichua tena sura yake halisi na isiyofichwa,” amesema Ayatullah Khamenei na kuongeza: “Uzoefu huu mbaya wa uhalifu na ahadi zilizovunjwa ni hati nyingine thabiti ya kutokuwa mwaminifu, kutokuwa na mantiki na uovu wa Marekani.”

Ayatullah Khamenei amesisitiza zaidi kwamba taifa la Iran na Kambi ya Muqawama wanayo “masomo yasiyosahaulika” kwa ajili ya adui Marekani, akitaja ujasiri wa wapiganaji wa Kiislamu na azma ya watu mashujaa wa kusini mwa Iran kama mifano hai ya ushujaa huo.

“Sasa kwa kuwa adui Mmarekani anataka kuchochea vita na kubeba gharama na fedheha kubwa zaidi, anapaswa kujua kwamba taifa pendwa la Iran na Mhimili wa Muqawama wanayo masomo yasiyosahaulika, masomo ambayo mfano wake wa karibuni umeonyeshwa na ushujaa wa wapiganaji wa Kiislamu na ujasiri wa watu wa kusini mwa Iran.”

Ayatullah Khamenei amesisitiza kwamba kulinda umoja wa kitaifa ni miongoni mwa “vipaumbele vya msingi zaidi vya nchi katika kipindi cha sasa.”

Ayatullah Mojtaba Khamenei ameongeza kuwa maafisa wa serikali, pamoja na wale waliojitolea kwa ajili ya Mapinduzi ya Kiislamu, Imam Khomeini na Kiongozi aliyeuawa shahidi, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, wana jukumu kubwa zaidi la kulinda umoja na mshikamano wa nchi.

Pia, amepongeza ushiriki usio kifani wa taifa la Iran katika mazishi na shughuli ya kumuaga Imam Ali Khamenei aliyeuawa shahidi katika shambulio la kushtukiza la Marekani na Israel, akiitaja idadi kubwa ya watu waliojitokeza katika tukio hilo kuwa ni “hamasa ya kihistoria na rekodi mpya ya kielelezo cha mwamko wa umma usio na kifani.”

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema mamilioni ya waombolezaji waliokusanyika kote Tehran, Qum, Mash’had na miji na vijiji vingine wamesifiwa na marafiki wa taifa la Iran na kuwaacha maadui katika hali ya bumbuazi, wenye hasira na wenye hofu.”

Vilevile ametoa shukrani kwa viongozi wakuu wa kidini, wasomi, wanaharakati wa masuala ya kitamaduni, kijamii na kisiasa, pamoja na taasisi za kiraia na kijeshi, kwa michango yao katika shughuli hiyo.

Ayatullah Mojtaba Khamenei pia amewashukuru maafisa na wawakilishi wa Mhimili wa Muqawama na harakati za Kiislamu kwa kushiriki katika mazishi ya Shahidi Ayatullah Khamenei na kuelezea matumaini kwamba wale wote walioshiriki, waliounga mkono, au kuonyesha mshikamano na tukio hilo la kihistoria watabarikiwa kwa neema na maombi ya Mwenyezi Mungu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *