Idadi ya watu waliofariki dunia kutokana na matetemeko mawili makubwa ya ardhi yaliyotikisa Pwani ya Karibiani nchini Venezuela mwezi uliopita imefikia 5,119, huku shughuli za uokoaji zikiendelea na mamlaka zikiendelea kuopoa miili kutoka kwenye vifusi vya majengo yaliyoporomoka.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Al- Jazeera likimnukuu Rais wa Bunge la Venezuela, Jorge Rodriguez,  waliofariki dunia wengi wanatoka jimbo la pwani la La Guaira, ambalo ndilo lililoathirika zaidi na maafa hayo.

Rodriguez amesema watu wengine 16,740 walijeruhiwa katika matetemeko hayo, lakini wengi wao tayari wameruhusiwa kutoka hospitalini baada ya kupatiwa matibabu.

Idadi ya vifo imeendelea kuongezeka kadiri vikosi vya uokoaji vinavyoendelea kuondoa vifusi na kufikia maeneo ambayo yalikuwa magumu kufikika katika siku za kwanza baada ya janga hilo.

Matetemeko hayo yenye ukubwa wa 7.2 na 7.5 yalitokea kwa tofauti ya chini ya dakika moja Juni 24, yakisababisha uharibifu mkubwa katika jimbo la La Guaira, lililopo kaskazini mwa mji mkuu wa Caracas.

Jimbo hilo lina uwanja mkuu wa kimataifa wa ndege wa Venezuela, bandari muhimu ya biashara na mamia ya majengo ya makazi ya ghorofa, mengi yakiharibiwa vibaya au kuporomoka kabisa.

Mamlaka zimesema zaidi ya mitetemeko midogo 1,300 imerekodiwa tangu kutokea kwa maafa hayo, huku takribani watu 20,000 wakiendelea kuishi katika makazi ya muda kutokana na kupoteza nyumba zao.

IMF yawashika mkono

Wakati juhudi za kukabiliana na athari za maafa hayo zikiendelea, Rais wa Mpito wa Venezuela, Delcy Rodriguez, ametangaza kuwa nchi hiyo imepata msaada wa dharura wa dola milioni 346 (sawa na Sh912 bilioni) kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).

Mkurugenzi Mkuu wa IMF, Kristalina Georgieva, amesema fedha hizo zimetolewa ili kusaidia kugharamia mahitaji ya haraka ya kibinadamu yanayotokana na maafa hayo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *