Dar es Salaam. Wakati mjadala kuhusu sababu za wahitimu wa vyuo vikuu kukosa ajira ukiendelea kushika kasi nchini, wasomi wamebainisha kubadili mitaala ya elimu pekee hakuwezi kumaliza tatizo hilo iwapo uchumi hautakuwa kwa kasi inayozalisha ajira za kutosha.

Miongoni mwa wanaochagiza hoja hiyo ni Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Profesa Raphael Chibunda, ambaye amesisitiza changamoto ya ajira kwa wahitimu si ya Tanzania pekee, bali ni tatizo linalozikabili nchi nyingi zinazoendelea, hivyo suluhisho linapaswa kuangalia kwa pamoja ubora wa elimu na uwezo wa uchumi kuzalisha nafasi mpya za kazi.

Akizungumza katika mahojiano aliyofanya katika podcast ya M&S, Profesa Chibunda amesema mara nyingi mjadala kuhusu elimu na ajira umejikita katika kuilaumu mitaala ya vyuo vikuu huku ukisahau hata wahitimu bora zaidi duniani hawawezi kupata ajira ikiwa uchumi hauna nafasi za kuwachukua.

“Nilikuwa kwenye mkutano nchini Nigeria tukijadili suala hili. Mtu mmoja akauliza, tukiwaleta leo wahitimu 2,000 kutoka MIT, Stanford au Oxford hapa Tanzania je, wote watapata ajira? Hakukuwa na jibu la moja kwa moja. Hapo ndipo tukagundua pamoja na kuboresha mitaala, lazima pia tujenge uchumi unaozalisha ajira,” amesema.

Amesema vyuo vikuu vina jukumu la kuzalisha wahitimu wenye maarifa na ujuzi, lakini haviwezi kuwa waajiri, hivyo ni wajibu wa taifa kujenga mazingira yanayochochea uwekezaji na ukuaji wa sekta zinazohitaji wataalamu hao.

Profesa Chibunda amesema sekta ya afya ni mfano unaoonesha uhusiano kati ya ukuaji wa sekta na ajira, akieleza madaktari wengi hupata ajira kwa sababu Serikali imeendelea kujenga hospitali na kupanua huduma za afya.

Kwa mujibu wa Profesa Chibunda, nchi inahitaji kuongeza idadi ya viwanda vinavyotumia teknolojia ya hali ya juu badala ya kutegemea viwanda vinavyofanya shughuli rahisi zisizohitaji wataalamu wengi wa elimu ya juu.

“Unaweza kuwa na kiwanda kinachoagiza mabati kutoka nje, kinaweka mikunjo na kuyakata. Hicho ni kiwanda, lakini kinahitaji wafanyakazi wachache wenye ujuzi wa kawaida. Wahitimu wa vyuo vikuu watafanya kazi gani kama hatuna viwanda vya teknolojia ya juu,” amehoji.

Amesema ili wahitimu wengi zaidi waajiriwe, Tanzania inapaswa kujenga uchumi unaohitaji wataalamu wa sayansi, teknolojia, uhandisi na ubunifu.

Profesa Chibunda amesema wakati wa mjadala wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ilielezwa ili kufikia malengo ya maendeleo, uchumi wa Tanzania unahitaji kukua kwa wastani wa asilimia 10 kwa miaka kadhaa mfululizo.

“Kwa sasa uchumi wetu unakua kwa wastani wa asilimia tano, wakati mwingine zaidi ya sita na mara chache umefika saba. Hilo linaonyesha bado tuna kazi kubwa ya kufanya kama tunataka kuzalisha ajira nyingi zaidi,” amesema Profesa Chibunda.

‘Uchumi unaozalisha’

Akizungumza na Mwananchi kuhusu hoja hiyo mhadhiri wa uchumi, Malcom Lambert amesema mjadala wa ajira kwa wahitimu unapaswa kuangalia upande wa mahitaji ya uchumi badala ya kuishia kwenye upande wa usambazaji wa nguvu kazi.

Amesema kwa miaka mingi Tanzania imekuwa ikiwekeza katika kuongeza idadi ya wahitimu wa vyuo vikuu, lakini ukuaji wa sekta zinazoweza kuajiri wataalamu hao haujaenda kwa kasi inayolingana.

“Unaweza kuzalisha wahitimu wengi wenye ujuzi mzuri, lakini kama uchumi hauna viwanda, kampuni za teknolojia, taasisi za utafiti na sekta zinazohitaji utaalamu huo, changamoto ya ajira itaendelea kuwepo,” amesema.

Amesema suluhisho la muda mrefu ni kujenga uchumi wa uzalishaji unaohitaji ujuzi wa juu badala ya kutegemea zaidi sekta zinazotoa ajira za kiwango cha chini.

Naye mtaalamu wa sera za elimu, Patric Msuya amesema maboresho ya mitaala ni muhimu lakini hayapaswi kuonekana kama tiba pekee ya tatizo la ajira.

Amesema vyuo vikuu vina wajibu wa kuhakikisha wahitimu wanakuwa na uwezo wa kutatua matatizo, kubuni na kujiajiri, lakini mazingira ya kiuchumi yanapaswa kuwawezesha kutumia ujuzi huo.

“Elimu inaweza kumwandaa mtu kuwa bora zaidi, lakini haiwezi yenyewe kuunda ajira bila kuwepo kwa mazingira ya uwekezaji na ukuaji wa sekta mbalimbali,” amesema Msuya.

Mtaalamu huyo ameeleza kuwa nchi zinazoendelea zimefanikiwa kupunguza tatizo la ajira kwa kuunganisha elimu, viwanda, utafiti na ubunifu, jambo ambalo Tanzania linapaswa kuliangalia kwa uzito.

Aonya dhidi ya upotoshaji kuhusu Veta

Katika hatua nyingine, Profesa Chibunda amesema kumekuwa na mtazamo unaopotosha wahitimu wengi wa vyuo vikuu wanapaswa kuelekezwa katika vyuo vya elimu na mafunzo ya ufundi stadi (Veta) kama suluhisho la ukosefu wa ajira.

Amesema Veta ina nafasi muhimu katika kuwajengea watu ujuzi wa kazi za mikono na taaluma mbalimbali za kiufundi, lakini haiwezi kuchukua nafasi ya elimu ya juu katika kuzalisha wataalamu wa kufanya tafiti, ubunifu na maendeleo ya teknolojia.

“Veta ni muhimu. Hata mimi nikitaka kujifunza kupaka rangi nyumba yangu naweza kwenda huko. Lakini nchi haiwezi kuwa na mafundi pekee. Tunahitaji pia watu wanaofikiri, wanaobuni na wanaotengeneza teknolojia mpya,” amesema.

Ametolea mfano maendeleo ya vifaa vya kisasa vya kiteknolojia, akisema mafundi wanaweza kuvitengeneza au kuviunganisha, lakini wabunifu wa teknolojia hizo ni wataalamu waliopitia elimu ya juu.

“Leo tuna kamera hizi tunazotumia. Wanaozikusanya wanaweza kuwa mafundi, lakini aliyebuni teknolojia ya jinsi mwanga unavyobadilishwa kuwa picha ni mtu aliyepata elimu ya juu,” amesema.

“Hatusikii sana malalamiko ya ajira kwa madaktari kwa sababu hospitali zinaendelea kujengwa na mahitaji yanaongezeka. Kama tungejenga viwanda na kupanua sekta nyingine kwa kasi kama hiyo, wahitimu wengi zaidi wangepata ajira,” amesema.

Akizungumzia hoja hiyo mhadhiri wa masuala ya maendeleo ya jamii, Hadija Mbando amesema uchumi unahitaji kada mbalimbali, wakiwemo mafundi wenye ujuzi wa vitendo pamoja na wataalamu wa elimu ya juu wanaofanya tafiti, kubuni teknolojia na kusukuma maendeleo ya viwanda.

“Hatuwezi kuwa taifa la mafundi pekee wala taifa la wasomi pekee. Tunahitaji mfumo unaounganisha ujuzi wa ufundi na maarifa ya juu ili kujenga uchumi unaoshindana,” amesema Hadija.

Amesema maendeleo ya nchi yanahitaji wataalamu wanaoweza kubuni mashine, kuanzisha teknolojia mpya, kuendesha tafiti na kutengeneza suluhisho la changamoto za kijamii.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *