INAELEZWA Yanga Princess iko katika hatua za mwisho kukamilisha usajili wa mshambuliaji kutoka Rwanda, Mutuyimana Sandrine baada ya kumpa mkataba wa miaka mitatu akitokea Inyemera WFC ya nchini kwao.
Sandrine anatua Jangwani baada ya kuwa miongoni mwa washambuliaji walioonyesha kiwango bora katika ligi ya wanawake ya Rwanda akifunga mabao 10 na kuongoza kwenye orodha ya wapachikaji mabao, sambamba na kuwa sehemu ya kikosi cha She Amavubi.
Ikumbukwe kabla ya Yanga kukubaliana naye kumsajili alikuwa tayari yuko nchini kwa zaidi ya mwezi mmoja akifanya majaribio na mazoezi na Yanga Princess, huku benchi la ufundi likipima uwezo wake kabla ya kumpa rasmi dili la kuitumikia timu hiyo kwa misimu mitatu.
Inaelezwa kipindi alichokuwa anafanya mazoezi na Wananchi hao kocha wa Yanga, Edna Lema ‘Mourinho’ amevutiwa na uwezo wake wa kufumania nyavu.
Mutuyimana anasajili Yanga kuziba nafasi ya Mrwanda mwenzie Jeannine Mukandayisenga ambaye aliuzwa hivi karibuni kwenda Wuhan Jiangda WFC inayoshiriki Ligi Kuu ya Wanawake China.